News

TANROADS YANG’ARA TUZO ZA NBAA

TANROADS YANG’ARA TUZO ZA NBAA

 

29 Novemba, 2024,

Dar es Salaam

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Mohamed Besta, Novemba 29, 2024 ameongoza timu ya TANROADS kupokea tuzo ya Uwasilishaji Bora wa Taarifa za Kifedha kwa kufuata viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika Sekta ya Umma (IPSAS), iliyotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA)

 

Tuzo hiyo ni ushaidi wa utendaji bora wa taasisi hiyo katika utayarishaji wa taarifa za fedha kwa kufuata viwango vya Kitaifa na Kimataifa.

 

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Mha. Besta amesema “Ni furaha kubwa kwangu na timu yangu kupata tuzo hii, ambayo imedhihirisha kwamba tunafuata vigezo vyote muhimu katika utayarishaji wa taarifa za kifedha zinazokidhi viwango vya ndani na vya kimataifa,”.

 

Hatahivyo, amesema wamejipanga kupanda hadi nafasi ya kwanza katika tuzo za mwaka 2024 kwa kuimarisha zaidi utayarishaji wa taarifa za kifedha na kuwapatia mafunzo  wahasibu wake.

 

Halikadhalika, amewapongeza watumishi wa TANROADS kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuhakikisha taarifa zao zinakaguliwa na kupitishwa na wakaguzi wa nje kwa viwango bora.

 

“Tumejipanga vizuri na tutaendelea kufanya kazi kama timu, ushirikiano huu ndio nguzo kuu ya mafanikio yetu,” amesema Mha. Besta.

 

Kwa upande wake, Mhasibu Mkuu, CPA Henry Mwakibete amesema TANROADS imeshika nafasi ya pili kati ya taasisi saba zilizoshiriki kwenye kundi la Wakala za Serikali.

 

CPA Mwakibete amesema hii ni mara ya kwanza kwa taasisi yake kushiriki kwenye mashindano haya, ambapo wahasibu wake wamekuwa wakipata mafunzo mbalimbali na kufuata mwongozo.