News

TANROADS yapongezwa kwa mchango wake wa kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja Manyara

TANROADS yapongezwa kwa mchango wake wa kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja Manyara

 

Manyara

18 Novemba, 2024

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga ameipongeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa juhudi zake za kuweka mipango mizuri ya kufungua mawasiliano ndani ya mkoa huo,  ambapo pia ameelezea umuhimu wa miradi ya ujenzi wa madaraja na barabara imechangia kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

 

Kauli hiyo ameitoa tarehe 18 Novemba, 2024 kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichoudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Mkoa, Bi. Maryam Muhaji.

Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo wa TANROADS Mkoa wa Manyara, Mhandisi Greyson Ndyamukama,akisoma ripoti ya mafanikio imeeleza kuwa ukarabati wa barabara ya Kateshi kwa kuziba viraka na kuweka tabaka la lami (overlay) imesaidia kuondoa changamoto kwa magari yanayopita kwenye barabara hiyo.

Mha, Ndyamukama pia, amesema kupitia bajeti ya mwaka 2024/2025, TANROADS imepanga kuendelea kuweka vibao vya alama za barabarani katika barabara zote wanazozisimamia, ili kupunguza ajali katika maeneo mbalimbali.

Pia amesema kupitia fedha za ufadhili wa Benki ya Dunia, TANROADS imepanga kutekeleza miradi ya ujenzi wa madaraja, matano ndani ya mkoa huo, iliyoathiriwa na mvua za El-nino.

Miradi hiyo inalenga kuboresha miundombinu na kurahisisha usafiri na usafirishaji kwa wananchi.

Kikao hicho kimeonesha dhamira ya Mkoa wa Manyara kuendelea kuboresha miundombinu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuchochea maendeleo endelevu katika Mkoa huo.