TANROADS yatoa vifaa vya uokozi kwenye jengo lililoanguka Kariakoo
18 Novemba, 2024
Dar es Salaam
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imetoa msaada wa vifaa mbalimbali vya uokozi kufuatia kuporomoka kwa jengo katika eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, siku ya Jumamosi, tarehe 16 Novemba 2024.
Vifaa hivyo vimewasilishwa ili kusaidia juhudi za uokoaji zinazoendelea katika eneo hilo. TANROADS imepeleka katika eneo hilo makalavati maalum yatakayowawezesha askari wa uokoaji kupita chini ya jengo haraka na kwa usalama zaidi.
Hatua hiyo imekuja kufuatia ombi lililotolewa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CGF), John Masunga, wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari tarehe 18 Novemba 2024.
Sambamba na makalavati, TANROADS pia imechangia vifaa vingine muhimu vikiwemo magari ya kubeba vifusi, vijiko (excavators), mashine ya kunyanyulia vitu vizito (crane), jenereta, na taa kubwa.
Vifaa hivi vinatarajiwa kufanikisha hatua mbalimbali za uokoaji na kuharakisha jitihada za kunusuru maisha na mali za wananchi. TANROADS inashirikiana na Watanzania wote kuwapa pole wale walioguswa na maafa haya, ikiwemo familia za waathirika. “Mungu awatie nguvu katika kipindi hiki kigumu,”
Mchango wa TANROADS katika juhudi za uokoaji ni kielelezo cha mshikamano wa kitaifa na uwajibikaji wa taasisi za umma wakati wa maafa. Tunatoa wito kwa wadau wengine kuendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha jitihada hizi zinafanikiwa kwa haraka na ufanisi.
Maafa haya ni changamoto kwa taifa zima, lakini kwa mshikamano na ushirikiano, tunaweza kukabiliana nayo na kurejesha matumaini kwa waathirika.