NAIBU SPIKA UJENZI WA DARAJA LA JANGWANI NI MATOKEO YA FALSAFA YA 4R YA RAIS SAMIA
Dar es Salaam
23 Oktoba, 2024
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu , amesema utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa daraja la Jangwani jijini Dar es Salaam ni mfano halisi wa matokeo na mafanikio ya falsafa ya 4R ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Falsafa hiyo inajumuisha: Reconciliation (maridhiano), Resilience (ustahimilivu), Reforms (mageuzi) na Rebuild (kujenga upya).
Amesema hayo tarehe 22 Oktoba, 2024 kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa daraja la Jangwani.
Mheshimiwa Zungu ameongeza kuwa, mradi huo ni sehemu ya juhudi za serikali za kuboresha miundombinu nchini, hatua inayochochea mabadiliko makubwa kwenye sekta hiyo.
Ameendelea kwa kusema kuwa, mabadiliko hayo yanatarajiwa kuimarisha uchumi wa nchi, kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa na abiria kwa haraka, hivyo kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi na maendeleo ya kijamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameeleza kufarijika kwa niaba ya wananchi wa Dar es Salaam kutokana na kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa daraja la Jangwani, akisema kuwa hatua hiyo inatoa mwanya kwa ujenzi wa daraja hilo muhimu kuanza.
Chalamila amesisitiza kuwa tukio la utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa daraja hilo, likichambuliwa kwa nadharia za kiuchumi na kijamii, lina faida kubwa kwa wananchi wa kawaida na historia imetengenezwa kupitia mradi huu.
Aidha, Chalamila ameongelea umuhimu wa barabara ya Kibada hadi Mwasonga, akieleza kuwa ni barabara ya kimkakati inayoelekea kwenye eneo lenye viwanda vingi wilayani Kigamboni, hivyo ni barabara muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Ameongeza kwa kusema kuwa daraja la Mzinga litakuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam na mikoa ya kusini.
Vilevile amekazia kuwa, usanifu wa barabara za jiji la Dar es Salaam unapaswa kuzingatia uchumi wa Dar es Salaam na changamoto za msongamano wa magari.