MKATABA WA UJENZI WA DARAJA LA JANGWANI WASAINIWA, BILIONI 97.1 KUONDOA KERO YA MAFURIKO NA MSONGAMANO DAR ES SALAAM
Dar es Salaam
22 Oktoba, 2024
Kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Jangwani jijini Dar es Salaam kunakwenda kuondoa kero ambazo wananchi wa Jiji la Dar es Salaam wamekuwa wakikumbana nazi kila mvua zinaponyesha hali inayopeleka barabara katika daraja hilo kufungwa.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Oktoba 22, 2024 na Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Innocent Bashungwa wakati wa hafla ya kutia saini mktaba wa ujenzi wa daraja la Jangwani jijini Dar es Salaam ambapo amesisitiza kuwa, wataendelea kuwasimamia wakandarasi ili kuhakikisha kwamba miradi inakamilika kwa wakati na kwa muda ambao wamekubaliana katika mkataba.
Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS ) itatekeleza ujenzi wa daraja hilo kwa lengo la kuondoa kero ya mafuriko na usumbufu kwa watumiaji wa barabara ya Morogoro hususani katika eneo hilo la Jangwani
Sambamba na hilo, Waziri Bashungwa amemushukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyotoa msukumo na maelekezo ya kukamilika hatua za ujenzi wa daraja hilo.
"Katika hili namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyotupa msukumo na maelekezo ya kwamba hataki kuona mwaka ukiisha bila ya mkandarasi wa kujenga daraja la Jangwani hajapatikana." alisema Waziri Bashungwa na kuongeza
"Mara ya mwisho kutembelea pale Jangwani wakati mvua zikinyesha niliwaambia wananchi kuwa, Rais wetu ni mtu wa vitendo na si mtu wa maneno mengi, na niliwaahidi kuwa kabla ya msimu wa mvua mwaka huu tutakuwa tushakamilisha masuala ya usanifu na kumpata mkandarasi"
Amefafanua kwa kusema kuwa, katika mradi huo, Daraja la Jangwani lenye urefu wa mita 390 na barabara za maingilio zenye urefu wa Mita 700 kwa pande zote za daraja zitajengwa na gharama ya mradi kwa ujumla ni shilingi bilioni 97.1
"Fedha hizo (bilioni 97.1) ni sehemu ya shilingi bilioni 125 ambazo tumewezeshwa na Mheshimiwa Rais kwa lengo la kurekebisha miundombinu ya Mkoa wa Dar es Salaam iliyoathiriwa na mvua za El-nino" alisisitiza Waziri Bashungwa.