DARAJA LA JANGWANI KUHARAKISHA MAENDELEO YA KIUCHUMI NA KIJAMII DAR ES SALAAM
Dar es Salaam
22 Oktoba, 2024
Ujenzi wa Daraja la Jangwani ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii Mkoani Dar es Salaam kwa kuboresha miundombinu ya usafiri, hususan barabara.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Oktoba 22, 2024 jijini Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa daraja hilo.
Mha. Besta ameongeza kwa kusema kuwa, gharama za jumla za ujenzi wa daraja hilo ni Shilingi bilioni 97.1, na TANROADS itasimamia utekelezaji wake kwa kuzingatia viwango vya kiufundi na muda uliopangwa.
Sambamba na hilo ametoa wito kwa mkandarasi kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokubalika.
Pia ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kufanikisha ujenzi huo, ambao unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri jijini Dar es Salaam.
Zabuni za ujenzi wa daraja hilo zilitangazwa Agosti 2, 2023, na kufunguliwa Oktoba 25, 2023 ambapo Kampuni ya China Communications Construction Company Limited ndiyo iliyoibuka mshindi kati ya wazabuni 11 waliojitokeza.
Kwa upande wa zabuni ya usimamizi wa mradi huo ilitangazwa Juni 12, 2023, na kushinda kampuni ya Leporogo Specialist Engineers ya Afrika Kusini kwa kushirikiana na Afrisa Consulting Ltd ya Tanzania na Dong Myeong Engineering Consultants & Architecture Co. Ltd ya Korea Kusini na itafanya kazi hiyo gharama ya Dola za Kimarekani Milioni 1.828, huku muda wa utekelezaji ukiwa miezi 24.
Upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi ulifanywa na Kampuni ya CDR International BV ya Uholanzi kwa kushirikiana na Kampuni Deltares ya Uholanzi na Wema Consultant ya Tanzania, kwa ufadhili wa Benki ya Dunia chini ya Programu ya Uboreshaji wa Miundombinu ya Usafiri katika Jiji la Dar es Salaam, kwa gharama ya Dola za Kimarekani 905,123.95.