News

MRADI WA BARABARA ZA KULIPIA WAWAVUTIA WAWEKEZAJI KUTOKA BURKINA FASO NA MALAYSIA

MRADI WA BARABARA ZA KULIPIA WAWAVUTIA WAWEKEZAJI KUTOKA BURKINA FASO NA MALAYSIA

16 Oktoba, 2024
Dar es Salaam

Makampuni makubwa ya ujenzi wa barabara, viwanja vya ndege, reli, na majengo makubwa kutoka nchi za ya Burkina Faso (SACBA – TP) na DMIA ya Malaysia yameonesha kuvutiwa na mradi wa barabara za kulipia, ambazo zitajengwa kupitia mfumo wa ujenzi wa ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Dodoma, Morogoro, na Mbeya.

Kwa nyakati tofauti, ujumbe kutoka nchi hizo umefanya mikutano na uongozi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), ulioongozwa na Mtendaji Mkuu Mhandisi Mohamed Besta, pamoja na mkutano mwingine ulioongozwa na Mtendaji wa Kituo cha PPP, David Kafulila.

Wataalamu wa ujenzi kutoka mashirika hayo wamewasilisha kazi walizofanya katika nchi zao na nchi zaidi ya kumi, wakionesha ufanisi wa miradi yao.

Mhandisi Besta amewaambia wajumbe kutoka Burkina Faso kuwa miradi ya barabara za kulipia itarahisisha maendeleo ya taifa na maisha ya watu binafsi kwa kupunguza msongamano wa magari, ambao umeongezeka kwa kiasi kikubwa hivi karibuni.

Akizungumza na ujumbe kutoka Malaysia, Kafulila alisisitiza kuwa lengo la miradi hiyo ni kukuza pato la taifa na kupunguza msongamano wa magari katika miji hiyo.

Miradi ya PPP inayotarajiwa kujengwa endapo wabia watapatikana ni pamoja na barabara ya Kibaha – Chalinze yenye urefu wa km 78.9; Chalinze – Morogoro km 84.9; Morogoro – Dodoma km 260; barabara ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam km 53.31; na barabara ya nje ya Dar es Salaam km 78.65.

Miradi mingine inayotarajiwa ni pamoja na daraja jipya la pili la Kigamboni na barabara ya Tunduma-Nakonde, inayopakana na nchi ya Zambia.