TANROADS YAWEKA TAA ZA BARABARANI KWENYE VITUO VYA MWENDOKASI KWA AJILI YA USALAMA WA WATEMBEA KWA MIGUU
Dar es Salaam
11 Septemba, 2024
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha watumiaji wote wa barabara ikiwemo watembea kwa miguu wanakuwa salama, miongoni mwa jitihada na njia hizo ni pamoja na uwekaji wa taa za kuongozea magari katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuzuia ajali, kupunguza msongamano na kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.
Kwa upande wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), taa hizo zimefungwa kwa ajili ya kuongoza magari katika makutano na vituo vya mabasi hayo huku lengo la kuweka taa hizo za barabarani ni kuzuia ajali kwa watembea kwa miguu pindi wanapovuka kwenda na kutoka kwenye vituo vya mabasi hayo.
Hayo yamesemwa na Meneja Mradi wa BRT Mhandisi Frank Mbilinyi ambapo amesisitiza kuwa, ujenzi wa miundombinu ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) wa awamu ya kwanza na awamu ya pili umekuwa tofauti.
Kwa awamu ya pili ya mradi wa BRT kutokea Gerezani-Mbagala utekelezaji wake unahusisha uwekaji wa taa za kuongozea magari ambazo zimeshawekwa katika barabara ya Kilwa (Kilwa Road) kuelekea Mbagala.
"Tunatumia njia nyingi kwa ajili ya kuzuia ajali ikiwemo kuweka taa mwanzo na mwisho wa kituo cha mabasi ya mwendokasi. Tunaamini kwamba inapowaka taa nyekundu madereva wengi wanaheshimu kuliko uwepo wa tuta pekee, kwani ukivuka taa nyekundu ni kosa kuliko kuvuka tuta" alisema Mhandisi Mbilinyi na kuongeza
"Kwa awamu ya kwanza ya mradi wa BRT tumeweka matuta kwenye kila kituo cha mabasi ya mwendokasi, mwanzoni mwa kituo na mwishoni wa Kituo ili yale magari yanayopita pembeni (ambayo siyo ya mwendokasi) kusimama na kumwezesha mtu kuvuka., na pia kuna zebra cross (kivuko cha watembea kwa miguu) mwanzoni mwa kituo na mwishoni mwa kituo ili mtembea kwa miguu avuke kwenda na kutoka kwenye kituo cha mabasi ya mwendokasi"
Akifafanua zaidi amesema, taa hizo zinadhibitiwa na pindi idadi kubwa ya watu wanapofika na kuhitaji kuvuka kwenda kwenye kituo, wanabonyeza kitufe kisha taa nyekundu itawaka kuzuia magari ili waweze kuvuka.
"Na hizo taa zinakuwa na muda maalumu tangu ulipobonyeza kitufe ambao ni makadario ya kutoka ng'ambo kuvuka kwenda kwenye kituo, na baada ya watu kuingia ndani ya kituo, zitawaka taa za kijani ili kuruhusu magari kuendelea kupita"
"Taa hizo hazitawaka kila mara tu pale unapotaka kuvuka kwani zimewekewa muda maalum kwa namna ambayo itafanya magari yasizuiwe kwa muda mrefu." alisisitiza Mhandisi Mbilinyi
Ameendelea kwa kusema kuwa, hatua hiyo ya kujenga miundombinu ya kisasa kwenye mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka ikiwemo taa za kisasa za kuongezea magari ni kwa lengo la kuzifanya barabara kuwa salama kwa watumiaji wote ikiwemo wenye vyombo vya moto na watembea kwa miguu.
TANROADS imefikia hatua hiyo ya kusimika taa hizo za kuongozea magari katika makutano na vituo vya mabasi ya mwendokasi kwa kuwa vituo vyake viko katikati ya barabara hivyo kumlazimu kila mtu avuke aingie katikati ya barabara ili aweze kuingia kwenye basi la mwendokasi au akitoka kwenye basi ni lazima pia avuke kwenda upande mwingine tofauti na hali ilivyo kwenye vituo vingine vya daladala, ambavyo viko pembeni ya barabara ambavyo sio hatarishi na ni na salama.
Kwa sasa Wakala imeweka taa pekee lakini miundombinu iliyopo kwenye vituo hivyo inaruhusu vifaa vingine vinavyoweza kudhibiti mwenendo wa magari, kuhesabu magari au idadi ya watu wanaoingia na kutoka. Miundombinu hiyo pia inawezesha kufungwa kwa vifaa vya kudhibiti uhalifu, wanaokwenda kasi na wanaovuka bila kusimama.
Serikali kupitia TANROADS inaendelea kuchukua jitihada za makusudi za kujenga na kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara lengo likiwa ni kuhakikisha watumiaji wa barabara wanakuwa salama.
Aidha, kwa sasa Wizara ya Ujenzi ipo katika hatua ya kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Usalama barabarani ili kuzingatia mambo mbalimbali yaliyobadilika ikiwemo teknolojia na kuzingatia malengo ya kimataifa ya kupunguza vifo vinavyotokana na ajali za barabarani kwa asilimia 50 ifikapo 2030