News

DARAJA LA MPIJI LILILOJENGWA NA TANROADS LAWA MKOMBOZI KWA WANANCHI WA MBWENI, KIHARAKA, MINAZI MIREFU, TUNGUTUNGU

DARAJA LA MPIJI LILILOJENGWA NA TANROADS LAWA MKOMBOZI KWA WANANCHI WA MBWENI, KIHARAKA, MINAZI MIREFU, TUNGUTUNGU

Dar es Salaam

08 Septemba, 2024

Mvua kubwa zilizonyesha kuanzia mwaka jana hadi mwaka huu zimepelekea uharibifu wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya madaraja na barabara katika maeneo mbalimbali nchini.

Miongoni mwa miundombinu iliyoharibiwa ni daraja la Mpiji linalounganisha Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kupitia vijiji vya Maputo na Kiembeni na kuleta adha kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo na maeneo jirani.

Kufuatia hali hiyo, Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam lilichukua hatua ya kujenga daraja la muda ili kufanya shughuli za usafiri na usafirishaji ziendelee katika eneo hilo.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi John Mkumbo amesema, waliamua kujenga daraja hilo ili wananchi wa maeneo hayo waendelee na shughuli za usafiri na usafirishaji ambapo sasa watumiaji wa magari na watembea kwa miguu wote wanapita bila changamoto yoyote.

Kufuatia ujenzi wa daraja hilo la muda, shangwe na furaha zimeibuka miongoni mwa wananchi wanaoishi maeneo ya Kiharaka, Kiembeni, Tungutungu, Minazi minane.

Miongoni mwa wananchi hao, ni Mchungaji Steven Kibiki amnbaye Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Jimbo la Kaskazini ambaye ameeleza hali halisi iliyokuwepo kabla na baada ya ujenzi wa daraja hilo.

"Kwa muda mfupi ambao nimekuwepo katika eneo la mto Mpiji ambao umekuwa ukisumbua sana na kuleta shida sana wakazi wa Kiharaka, Kiembeni, Tungutungu, Minazi minane kabla ya daraja hili kujengwa" amesema Kibiki na kuongeza



… "Kuhusu juhudi mbalimbali zilikuwa zikifanyika, ikiwemo kuweka madaraja madogo madogo, madaraja yalikuwa yanajengwa lakini yalikuwa yanavunjika na wakati mwingine mwingine wanaweka hadi mitumbwi ya kuvushia watu na kupelekea watu kupata athari mbalimbali ikiwemo kupoteza mali zao".



Kufuatia ujenzi wa daraja hilo adha hizo zimetoweka na ahueni kubwa imepatikana kama alivyoeleza mchungaji huyo

 

"Baada ya daraja hili kujengwa imekuwa ni msaada mkubwa sana kwa watembea kwa miguu na wanaotumia magari, hata watu waliokuwa wamehama kutokana na changamoto ya daraja ilivyokuwa imepelekea baadhi yao vyombo vyao vya usafiri kuviacha ng'ambo nyingine nao wamerejea katika maeneo yao na pia idadi ya wakazi katika maeneo haya imeongezeka" alisisitiza Mchungaji Kibiki

Kwa upande wake Njiku Salumu Kisuda, akiongea kwa niaba ya wakazi wa Mbweni, mtaa wa Maputo ametoa shukrani zake kwa serikali kupitia TANROADS kwa kujenga daraja hilo ambalo limeondoa changamoto zilizokuwa zikiwapata ikiwemo kutumia mitumbwi kwa ajili ya kuvuka kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine.

Mbali na shukrani hizo Bw. Kisuda ameiomba serikali kulijenga daraja la Mpiji ili adha walizokuwa wakizipata zisitokee tena kwa mara nyingine.

"Pia tunashukuru kwa kutuwekea taa ambazo zinatuwezesha kupita hata nyakati za usiku na kuimarisha usalama" alihitimisha Kisuda

Ikumbukwe, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari imeelekeza kiasi cha Shilingi Bilioni 840 (Dola za Marekani Milioni 325) katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja na makalvati yaliyoharibiwa na mvua kubwa za El-Nino na Kimbunga Hidaya ambapo maandalizi ya utekelezaji huo yanaendelea.