TANROADS YASHIRIKI KONGAMANO LA 16 LA UNUNUZI WA UMMA LA AFRIKA MASHARIKI, IKIJIVUNIA KUFANYA MANUNUZI YALIYONYOOKA
Arusha
09 Septemba, 2024
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeshiriki Kongamano la 16 la Ununuzi wa Umma Afrika Mashariki lilioanza Septemba 9, 2024 jijini Arusha kwa kutambua kuwa, sehemu kubwa ya kazi zinazofanywa na Wakala zinahusisha manunuzi hivyo kupitia kongamano hilo manufaa makubwa yatapatikana ikiwemo kupata uelewa wa namna TEHAMA inavyoweza kutumika kurahisisha taratibu za manunuzi.
Akiongea katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya TANROADS Mhandisi Amin Mcharo amesema, TANROADS inajihusisha na manunuzi mbalimbali ikiwemo ununuzi wa kazi za ujenzi, ununuzi wa huduma za ushauri wa kiuhandisi, ununuzi wa vifaa kwa ajili ya ofisi za Wakala na kwa nyakati zote wamekuwa wakizingatia taratibu zote husika.
Mhandisi Mcharo ameongelea ushirikiano uliopo baina ya TANROADS na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kuwa ni mkubwa, ushirikiano ambao umepelekea TANROADS kupata sifa ya kufanya manunuzi katika njia iliyonyooka.
"Ushirikiano wetu na PPRA ni mkubwa sana na hii ni kutokana na shughuli za manunuzi katika TANROADS kuwa ni kubwa sana, na siku zote tumekuwa tukishirikiana nao. PPRA wamekuwa wakithamini namna tunavyofanya manunuzi yetu katika njia zilizonyooka" alisema Mhandisi Mcharo
Mwenyekiti huyo wa Bodi ya TANROADS amezitaja faida wanazozipata kupitia mfumo mpya wa kielektroniki wa manunuzi ya umma wa NeST kuwa ni kuwezesha sekta ya manunuzi kuimarika zaidi katika usawa na uwazi na kuwezesha thamani ya fedha kupatikana.
"Faida ambazo sisi TANROADS tunazipata kupitia mfumo wa NeST ni pamoja na kupatikana kwa uwazi kwenye taratibu za manunuzi, kusaidia kuondoa mianya ya rushwa kwa sababu hakuna kuonana moja moja kati ya mnunuzi na anayetoa huduma. Pia itatuwezesha kupata thamani ya fedha (value for money)" aliongeza Mhandisi Mcharo
Kongamano hilo limefunguliwa Septemba 09, 2024 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Dotto Biteko kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo linatarajiwa kufikia kilele chake Septemba 12, 2024.
Kwa upekee wake, TANROADS imepata tuzo kutokana na ushiriki wake katika hatua za maandalizi na kufanikisha kufanyika kwa kongamano hilo muhimu kwa mustakabali wa sekta ya manunuzi kwa manufaa ya Taifa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.