TANROADS YAELEZA NAMNA MFUMO WA NeST ULIVYOWANUFAISHA KATIKA SEKTA YA MANUNUZI
Arusha
10 Septemba, 2024
Mfumo mpya wa kielektroniki wa manunuzi ya umma wa NeST umetajwa kuwa ni mfumo rahisi kwa mtumiaji ukiwa na sifa ya kutoa mwongozo na hivyo kutokuwa kikwazo kwa mtumiaji wa mara ya kwanza huku ukiimarisha uwazi, kupunguza malalamiko na kuongeza uwajibikaji.
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kama taasisi ya serikali, mfumo huo umewanufaisha kwa punguza gharama kubwa za kuzalisha makabrasha ya zabuni na muda wa uzalishaji wa nyaraka pamoja na kuepuka makosa ya kiununuzi.
Hayo yamesemwa Septemba 10, 2024 na Kaimu Meneja wa Udhibiti wa Mikataba TANROADS akimwakilisha Mkurugenzi wa Ununuzi na Mikataba Mhandisi Mussa Kaswahili kwenye Kongamano la 16 la Ununuzi wa Umma Afrika Mashariki linaloongozwa na Kaulimbiu: “Digitalization for Sustainable Public Procurement” (Matumizi ya Dijitali kwa Ununuzi wa Umma Endelevu).
Mhandisi Kaswahili amesema, hapo awali
wakati mfumo wa kawaida wa manunuzi wa makaratasi ukitumika changamoto nyingi zilikuwa zikijitokeza ikiwemo kushuhudia wakandarasi na wazabuni wakiandaa nyaraka nyingi sana na hivyo kupata changamoto ya gharama za uandaaji na muda.
"Lakini kwa kupitia mfumo wa NeST, mzabuni hatakuwa na haja ya kuzalisha nakala nyingi ili aweze kuwasilisha, badala yake anakaa ofisini kwake, anapata taarifa za matangazo yetu ya zabuni, atajaza na kuwasilisha maombi yake akiwa huko alipo" alisema Mhandisi Kaswahili
Akifafanua zaidi amesema, serikali imewekeza nguvu kupitia Sheria ya Manunuzi No. 10 ya mwaka 2023 pamoja na kanuni zake za mwaka 2024 kwa kuwajali na kuwapa kipaumbele wakandarasi na wahandisi washauri kwa kuanisha kwamba ni lazima kuwepo miradi kwa ajili ya wakandarasi wazawa.
"Sasa tunakwenda kuwainua wakandarasi wazawa na kuwaimarisha wahandisi washauri kutokana na kuwepo kwa fursa kubwa ya kutekeleza miradi ya kitaifa ya kimkakati kote nchini" aliongeza Mhandisi Kaswahili
Kufuatia hilo, Mhandisi Kaswahili ametoa rai kwa wakandarasi na wahandisi washauri wazawa kuunganisha nguvu ili waweze kupata zabuni za miradi mikubwa hapa nchini kama ambavyo makampuni ya kigeni yanavyoungana ili kuweza kupata miradi mikubwa.
Katika hatua nyingine, ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake kwa Wakala kupitia Wizara ya Ujenzi na kwamba wameyapokea maelekezo hayo na wako tayari kuyatekeleza lengo likiwa ni kuwahudumia wananchi ipasavyo na kutekeleza azma ya Serikali ya kuboresha miundombinu mbalimbali kote nchini.
Kongamano la 16 la Ununuzi wa Umma Afrika Mashariki lilioanza Septemba 09-12, 2024 llimewakutanisha wadau wa sekta ya ununuzi wa umma kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambazo ni mwenyeji Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini na Uganda.
Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamepata fursa ya kujadili na kubadilishana uzoefu katika sekta ya ununuzi wa umma katika ukanda huo.
TANROADS inawakaribisha wananchi na wafanyabiashara wote katika banda lao kwenye kongamano hilo ambapo watakutana na wataalamu mbalimbali wanaotoa elimu kuhusu kazi mbalimbali zinozozfanywa na Wakala ikiwemo kuhusu matumzi ya hifadhi ya barabara na mizani.