News

WANANCHI WA LIWALE NA NACHINGWEA WALILIA BARABARA

Wananchi wa wilaya ya Liwale na Nachingwea mkoani Lindi wameiomba Serikali kuhakikisha inaanza ujenzi wa barabara ya Liwale - Nachingwea (Km 129) kwa kiwango cha lami ili kutatua changamoto za usafirishaji wa abiria na mazao katika wilaya hizo.

 

Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, Mkuu wa wilaya ya Liwale Bi. Sarah Chiwamba amesema kuwa wanachi wake wanaamini kuwa Liwale itafunguka kibiashara na kiuchumi endapo itakuwa imeimarishwa katika mtandao wa barabara ambazo zitaiunganisha wilaya hiyo na wilaya jirani pamoja na nchi kwa ujumla.


"Naamini barabara hizi zikikamilika wilaya hii na mkoa wetu utaendelea kiuchumi kwani suala la miundombinu ya barabara imekuwa ni kilio cha muda mrefu katika wilaya yetu", amesema Mkuu wa Wilaya.

 

Aidha, Bi. Sarah amefafanua kuwa wananchi wengi katika wilaya hiyo ni wakulima, hivyo wamekuwa wakitumia miundombinu ya barabara kusafirisha mazao ya korosho na ufuta yanayozalishwa kwa wingi kuelekea maeneo mbalimbali ya nchi.


Kwa upande wake, Naibu Waziri huyo anayeshughulikia masuala ya Ujenzi, amewataka wataalamu wote wa masuala ya ujenzi nchini kupitia Sera ya Ujenzi ya mwaka 2003 ambayo itawasaidia kuwapa mwongozo katika utekelezaji wa majukumu yao katika kutoa huduma bora kwa jamii.


Ameongeza kwa wataalam wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kuwa wabunifu katika ujenzi wa barabara zao ili kuondoa dhana potofu iliyopo dhidi ya usimamizi wa barabara kati yao na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

 
"TANROADS na TARURA shirikianeni katika kuhakikisha mnawajengea wananchi miundombinu iliyobora, kusiwepo na utofauti kati ya barabara mnazozisimamia", amesema Naibu Waziri huyo.


Ametoa wito kwa uongozi wa TANROADS mkoani Lindi kuhakikisha kuwa wanaboresha maeneo yote ya barabara ambayo ni korofi ili yaweze kupita kiurahisi katika kipindi chote cha mwaka.

 

Naye, Meneja wa TANROADS mkoani Lindi, Mhandisi Isaack Mwanawima, amemhakikisha Naibu Waziri Kwandikwa kuendelea na mpango wa matengenezo ya barabara kwa kiwango cha lami ili kufungua fursa mbalimbali katika mkoa huo.

 

Naibu Waziri Kwandikwa yupo katika ziara ya kikazi mkoani Lindi kujionea hali halisi ya mtandao wa barabara katika mkoa huo ambapo pamoja na mambo mengine ametembelea na kukagua daraja la Nandanga lenye urefu wa mita 30 ambalo lipo kwenye mto Lukuledi katika barabara ya wilaya ya Luchelegwa- Ndanda inayounganisha wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi na Masasi mkoa wa Mtwara ili kujionea miundombinu yake.


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.