News

MIUNDOMBINU YA BARABARA NA MADARAJA YAENDELEA KUBORESHWA KUPUNGUZA AJALI

MIUNDOMBINU YA BARABARA NA MADARAJA YAENDELEA KUBORESHWA KUPUNGUZA AJALI

Dodoma

29 Augusti, 2024

Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu bora ya barabara na madaraja ya kisasa ili kupunguza ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikikatisha uhai wa wananchi wengi.

 

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, Agosti 29, 2024 wakati akifunga Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani ambayo kitaifa yamefanyika jijini Dodoma.

 

“Serikali inaendelea kuchukua jitihada za makusudi za kujenga na kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, reli, kuweka mifumo ya kufuatilia mwenendo wa madereva wa mabasi kwa kuwa na dereva zaidi ya mmoja kwenye mabasi, lengo la jitihada hizi ni kuhakikisha watumiaji wanakuwa salama wawapo safarini”, amesema Kihenzile.

 

Kihenzile ameongeza kuwa elimu iliyotolewa katika Wiki hiyo kuanzia tarehe 26 – 30 Agosti, 2024 itakuwa ni chachu ya mabadiliko kwa madereva wa vyombo vya moto, wapanda pikipiki na makundi yote ya watumiaji wa barabara.

 

Kwa upande wake, Mhandisi Omari Kinyange kutoka Kitengo cha Usalama na Mazingira, Wizara ya Ujenzi, amesema kuwa Wizara hiyo ipo katika hatua ya kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Usalama barabarani ili kuzingatia mambo mbalimbali yaliyobadilika ikiwemo Teknolojia na kuzingatia malengo ya Kimataifa ya kupunguza vifo vinavyotokana na ajali za barabarani kwa asilimia 50 ifikapo 2030. 

 

Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani Kitaifa imefanyika jijini Dodoma kuanzia tarehe 26 hadi 30 Agosti, 2024 ambapo wananchi na wadau mbalimbali wamepata elimu ya Usalama Barabarani na kuwakumbusha matumizi sahihi ya barabara ili kupunguza matukio ya ajali nchini.