News

TANROADS YATOA ANGALIZO KWA WANAOFANYA MAZOEZI KWENYE MADARAJA YA JUU

TANROADS YATOA ANGALIZO KWA WANAOFANYA MAZOEZI KWENYE MADARAJA YA JUU

 

Dodoma

29 Agosti, 2024

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), imewataadharisha wananchi wanaotumia madaraja ya juu (Flying over) kwa kufanya mazoezi wanaweza kujeruhiwa au kupoteza maisha kwa kugongwa na magari  au pikipiki zinazopita kwenye madaraja hayo.

 

Kauli hiyo imetolewa tarehe 28 Agosti, 2024 na Meneja wa Kitengo cha Usalama Barabarani, Mhandisi George Daffa wakati akitoa elimu ya masuala mbalimbali kwa wananchi waliotembelea banda la maonesho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama yenye kaulimbiu ya “Endesha Salama Ufike Salama” yanayoendelea katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

 

Mha. Daffa amewataka baadhi ya wananchi waliogeuza maeneo ya madaraja ya juu  kuwa ni sehemu ya kufanyia mazoezi, waache mara moja kwa ajili ya usalama wao, kwa kuwa madaraja hayo yamejengwa kwa lengo la kupita vyombo vya moto ambavyo vinaweza kuwajeruhi au kufa.

 

“Haya madaraja ya juu (flying-over) yamejengwa kwa ajili ya kupita magari na lengo kuu ni la kupunguza msongamano lakini sasa wapo watu wameyageuza kuwa maeneo ya mazoezi wakati wanatakiwa wafanye kwenye viwanja vya michezo, ninatoa wito wananchi wasifanye mazoezi hapo wanaweza kugongwa na magari au pikipiki,” amesema Mha. Daffa.

 

Pia Mha. Daffa amesema wakati akitoa elimu ya eneo la uhifadhi wa barabara kuwa ni mita 30 kutoka katikakti ya barabara kwa pande zote mbili, hivyo wananchi wanaotaka kujenga wanatakiwa kuhakikisha wanakaa umbali wa mita hizo au zaidi ili kujiepusha na madhara ya kuvunjiwa bila kulipwa fidia.

 

“Kwanini tunasema ujenge nyuma ya umbali wa mita 30 kutoka kwenye mstari wa katikati ya barabara kwa kila upande, kuna madhara makubwa yakiwemo ya magari kuacha njia na kugonga nyumba yako na aidha kujeruhi au kuua watu waliokuwemo ndani ya nyumba husika, pia nyumba hiyo itavunjwa na mamlaka bila kulipwa fidia kwa mjengaji aliyevamia maeneo hayo yasiyoruhusiwa kwa makazi ya kudumu,”, amesema Mha. Daffa.

 

Halikadhalika, Mha. Daffa amewaeleza wananchi hao faida za kupita juu ya madaraja ya juu ya waenda kwa miguu kuwa yanawaepusha na kugongwa na vyombo vya moto vya magari na pikipiki.

 

Hatahivyo, amekemea baadhi ya wananchi ambao bado wanalazimisha kupita chini ya barabara kama ilivyokuwa awali, ilihali tayari kumewekwa uzio ili wasipite chini, wanaweza kupoteza maisha kwa kugongwa na vyombo vya moto.

 

Mha. Daffa amesema TANROADS wamekuwa wakipata madhara ya kuibiwa kwa alama za barabarani zikiwemo kingo za madaraja kunakofanywa na watu wasiojulikana, na kwenda kuuza kama chuma chakavu, bila kutambua madhara yake ikiwemo ya kudhoofisha uchumi wa  nchi.

 

Kwa upande wa magari ya mizigo, amesema TANROADS inajenga barabara zinazodumu takribani miaka 20 lakini wapo wamiliki wenye kuzidisha mizigo kwa makusudi kwenye magari yao ambayo yanaharibu barabara hiyo.