TANROADS IRINGA YAWEKA MIKAKATI YA KUPUNGUZA AJALI NA MSONGAMANO KATIKA MLIMA KITONGA
Iringa
28 Agosti, 2024
Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inatekeleza mradi wa upanuzi wa mlima Kitonga kwa lengo la kupunguza msongamano na ajali, kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji katika mlima huo pamoja na kukuza uchumi kutokana na ukweli kwamba barabara inayopita katika mlima huo (barabara ya Tanzam) inatumika na nchi zaidi ya saba.
Katika kuhakikisha azma hiyo inafikiwa, Wakala imekuja na suluhisho la muda mfupi na muda mrefu.
Katika suluhisho la muda mfupi, jumla ya Mita 1600 (Km 1.6) katika Mlima Kitonga zitaongezwa, ili kupunguza ajali na foleni katika zilizokuwapo awali..
Hayo yamesemwa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa, Mhandisi Yudas Msangi na kusisitiza kuwa kazi ya upanuzi wa kona za Mlima Kitonga itakwenda sambamba na uwekaji wa vioo kwenye kona kali.
"Kwa sasa mkandarasi kampuni ya Mtwivila Traders and Construction Company Limited anaendelea na kazi ya upanuzi wa kilometa 1.6, tukimaliza kutakuwa na barabara tatu ambazo zitawezesha magari kupita kwa kupishana" amesema Mha. Msangi
Kwa suluhisho la muda mrefu, Mha. Msangi amesema, wamepata mhandisi mshauri ambaye atafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika Km 7.6 za Mlima Kitonga.
"Mhandisi mshauri katika hadidu za rejea tulimwambia afanye mambo tuliyoyapendekeza na mengine atakayoona yanafaa, mambo hayo ni pamoja na
pendekezo la kujengwa kwa barabara ya mchepuo Mlowa – Mifugo – Mlafu hadi Ilula, kupanua barabara iliyopo, kupanda handaki la barabara (Tunnel) na kuchoronga barabara ya chini kwa chini inayoweza kutokea juu" alisisitiza Mhandisi Msangi.
Amesema kuwa, mapendekezo hayo yatafanyiwa kazi na kufikia mwezi Desemba, mwaka huu mkandarasi huyo atatoa majibu ya nini kifanyike katika Mlima Kitonga kwa lengo la kupunguza ajali, msongamano na kuwezesha magari kupita kwa kupishana na kwa muda mfupi.
Mbali na mradi huo, miradi mingine ya ujenzi wa miundombinu ya barabara inayoendelea kutekelezwa katika Mkoa wa Iringa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa barabara ya mchepuo ya Iringa (Iringa Bypass) inayoanzia Kihesa - Kilolo kwenda Igumbilo.
Katika utekelezaji wa mradi Iringa Bypass mambo kadhaa yatafanyika ikiwemo, kuweka barabara za kupanda (climbing lane), taa za barabarani, kuweka maegesho ya malori yenye urefu wa mita 600 pamoja na kuipanua barabara hiyo na kujengwa kwa lami ngumu (SP 12.5 na SP 19.5) lengo likiwa ni kuiwezesha barabara hiyo kuhimili magari yenye uzito mkubwa na kuondoa msongamano.