KAMATI YA MAWASILIANO, ARDHI NA NISHATI YA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR, YASIFU UWEKEZAJI WA UJENZI WA BARABARA NA VIWANJA VYA NDEGE NCHINI
Dodoma
30 Agosti, 2024
Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar leo Ijumaa Agosti 30, 2024, imetembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato pamoja na mradi ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami wa njia nne ya mzunguko (Outer Ring Road) nje ya jiji la Dodoma yenye urefu wa Km. 112.3, miradi ambayo inatekelezwa na Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) ambapo kamati hiyo imeeleza kupata mafunzo lukuki kutoka kwenye miradi hiyo.
Akiongea mara baada ya kutembelea miradi hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Yahya Rashid Abdallah amesema, miongoni mwa mambo ambayo kamati yake imejifunza ni pamoja Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TANROADS kuwa na mipango ya muda mrefu wa matumizi ya miundombinu wanayoijenga jambo ambalo wamesema pindi watakaporudi Zanzibar watakwenda kuishauri serikali katika eneo hilo.
"Moja ya jambo kubwa tulilojifunza ni kwamba, wenzetu wanapotengeneza uwanja wa ndege au miundombinu ya barabara hawaangalii mipango ya muda mfupi bali wanaangalia mipango ya muda mrefu kwa matumzi ya viwanja vya ndege na barabara" alisema Mheshimiwa Yahya na kuongeza
"…Tutakwenda kuishauri serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar iwe na mpango wa muda mrefu katika matumizi ya viwanja vyetu vya ndege lakini hali kadhalika katika upande wa barabara tunazozijenga, hivyo ndivyo ilivyo lakini tutakwenda kusisitiza haya," amesema Mheshimiwa Yahya.
Halikadhalika, ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake kubwa za uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani amesema, Wakala kwa kushirikiana na wahandisi washauri wa miradi watahakikisha ujenzi wa miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa viwango kwa kuwa miradi hiyo ni ya kimkakati yenye manufaa kwa Mkoa wa Dodoma na Taifa kwa ujumla.
Pia, Mha. Zuhura ameshukuru mchango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo miradi ya kimkakati mkoani humo.
"Tunaishukuru serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani ujenzi wa mradi huu unafanyika chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa upande wa ujenzi wa majengo na miundombinu ya barabara lakini vilevile serikali inachangia kwa kulipa fidia wananchi waliopisha mradi" alisema Mha. Zuhura
Amesema kuwa, kutokana na malipo ambayo Serikali ya Awamu ya Sita ambayo imekuwa ikiyatenga kwa ajili ya miradi hii, wana imani itakamilika ndani ya muda uliowekwa ili iende kutatua changamoto kwenye shughuli za usafiri na usafirishaji wa anga na kuwarahisishia wananchi na watumiaji wa barabara kufika katika maeneo yao kwa wakati na hivyo kukuza uchumi wa jiji la Dodoma na Taifa kwa ujumla.
Naye msimaminzi wa mradi uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato mkoani Dodoma kutoka TANROADS, Mha. Mahona Luhende amesema, mradi huo unaogharimu takribani shilingi Bilioni 300 unatekelezwa na wakandarasi wawili, mkandarasi mmoja anayejenga miundombinu ya barabara ya kuruka na kutua kwa ndege na mkandarasi mwingine anayejenga miundombinu ya majengo., ambapo inatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, mwaka 2025
"Upande wa ujenzi wa miundombinu ya barabara umefikia asilimia 72 hadi sasa huku ujenzi wa miundombinu ya majengo umefikia asilimia 39. Kipindi cha utekelezaji wa miradi yote miwili ni miezi 36,” amesema Mha. Luhende
Mha. Herman Laswai ambaye ni mratibu wa miradi ya AfDB na msimamzi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje wa Jiji la Dodoma amesema, ujenzi wa barabara hiyo utafanyika kwa awamu mbili ya kwanza inahusisha ujenzi wa barabara ya kuanzia Nala-Veyula-Barabara ya Arusha-Mtumba-Ihumwa (bandari kavu) kikiwa na urefu wa Km 52.3, ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 80.6, hatua ya pili inaanzia Ihumwa (bandari kavu)-Matumbulu-Nala chenye urefu wa kilometa 60 ujenzi wake umefikia asilimia 76.6