SERIKALI KUENDELEA NA UJENZI WA BARABARA YA KWIMBA – MAGU KM 71
Dodoma
28 Agosti, 2024
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya Nhungumalwa-Ngudu-Magu Km 71 mkoani Mwanza kwa kiwango cha lami na ujenzi wake unatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mha. Kasekenya amesema hayo leo tarehe 28 Agosti, 2024 bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali aliloulizwa na Mhe. Mery Masanja, Mbunge wa Viti Maalum akitaka kujua ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
“Mh.Spika Serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo inayoungaisha majimbo matatu ikiwemo jimbo la Kwimba, Sumve na Magu, sehemu ya mzunguko eneo la Itandula tayari imekalika na Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa ujumla” amesema Mha. Kasekenya.
Mha. Kasekenya ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2022/2023 mkataba wa ujenzi wa sehemu ya barabara Km 10 ulisainiwa mwezi Mei na Mkandarasi yupo katika maandalizi ya kuanza ujenzi.
Mbunge huyo amezungumzia umuhimu wa barabara hiyo yenye tija kwa wananchi inayopitisha shughuli nyingi za kiuchumi na kibiashara ambapo amesema ikikamilika itarahisisha usafirishaji wa mazao kwa wafanyabiashara wa mkoa huo.
Halikadhalika, Naibu Waziri Mha. Kasekenya amesema Serikali inaendelea kutekeleza majukumu yake ya ujenzi wa miundombinu ambapo imekamilisha kazi ya upembuzi na usanifu wa kina wa barabara ya Ntaba-Ipinda-Mbambo km 18 kwa kiwango cha lami na ujenzi wake utaanza.
Mha. Kasekenya ameeleza hayo alipokuwa akijibu swali la Mhe.Atupele Mwakibete Mbunge wa Jimbola Busokela aliuliza Je ni lini zabuni ya ujenzi wa barabara ya Mbambo - Ntaba hadi Ipinda kiwango cha lami itatangazwa.