News

TAKRIBANI BILIONI 300 ZIMETENGWA KWA AJILI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA BARABARA NA MADARAJA KATIKA MKOA WA TANGA

TAKRIBANI BILIONI 300 ZIMETENGWA KWA AJILI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA BARABARA NA MADARAJA KATIKA MKOA WA TANGA

Tanga

25 Agosti, 2024

Miradi ya ujenzi wa barabara inayotekelezwa na Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Tanga katika ushoroba wa barabara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki imewezesha kutoa fursa za ajira zaidi ya 1,200 kwa Watanzania hadi sasa huku kukamilika kwake kunatajwa kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta za kilimo, uvuvi na utalii.



Hayo yamesemwa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga, Mhandisi Danstan Singano ambapo amewataka wananchi kuwa walinzi wa kwanza wa miundombinu ya barabara ili barabara zinazojengwa zilete tija kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.



Mhandisi Singano amesema, miradi hiyo ambayo imegawanyika katika sehemu nne imetengewa fedha za kutosha kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wake.



"Hadi sasa takribani Bilioni 300 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hii, tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wasaidizi wake Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango,  Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa uongozi wa Wizara ya Ujenzi ukiongozwa na Mheshimiwa Innocent Bashungwa kwani wamekuwa watu wa kutupa msaada mkubwa sana katika utekelezaji wa miradi hii. Tunawashukuru sana" alisema Mhandisi



Vilevile Meneja huyo wa TANROADS Mkoa wa Tanga, amewataka wananchi wa mkoa huo na kote nchini kuchukulia miundombinu ya barabara kama mojawapo ya rasilimali kubwa na muhimu katika kuwaletea maendeleo wananchi hivyo kufanya uharibifu au wizi wa miundombinu hiyo ni kutowatakia mema wananchi na Taifa kwa ujumla.



"Unapoharibu au kuiba miundombinu ya barabara, mimi nakuhesabia wewe kama ni muuaji, kwasababu alama za barabarani zinapowekwa ni kwa ajili ya kutoa tahadhari kwa watumiaji wa barabara kwenye maeneo mengi ikiwemo maeneo hatarishi kwa ajali. Sasa unapoondoa alama za barabarani, mtu anapotumia barabara hiyo hatojua kuwa huko mbele kama kuna sehemu hatarishi ili aweze kuchukua tahadhari, hilo linachangia kusababisha ajali ambazo zinagharimu maisha ya watu na kuharibu mali zao." alisisitiza Mhandisi Singano

 

Kwa upande wake Mhandisi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Tungamaa - Mkwaja-Mkange, Mhandisi Julius Msofe amesema, ujenzi barabara hiyo umefikia asilimia 40, ikiwa ni sehemu ya tatu ya miradi wa ujenzi miundombinu iliyopo katika ushoroba wa barabara ya Afrika Mashariki inayoanzia Lungalunga nchini Kenya hadi Makurunge wilayani Bagamoyo.



Mhandisi Msofe ameendelea kwa kusema kuwa, sehemu hiyo ya tatu imepata ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.



Mradi wa ujenzi wa barabara ya Tungamaa - Mkwaja-Mkange yenye urefu wa Kilometa 92.5 kwa kiwango cha lami unatekelezwa na mkandarasi kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Coorporation kutoka nchini China kwa gharama ya shilingi Bilioni 94.