News

UJENZI WA BARABARA YA AFRIKA MASHARIKI KUTOKA LUNGALUNGA (KENYA) HADI MAKURUNGE – BAGAMOYO KUFUNGUA FURSA ZA KIUCHUMI

UJENZI WA BARABARA YA AFRIKA MASHARIKI KUTOKA LUNGALUNGA (KENYA) HADI MAKURUNGE – BAGAMOYO KUFUNGUA FURSA ZA KIUCHUMI

 

Tanga

20 Agosti, 2024

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inatekeleza miradi minne mikubwa ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja katika mkoa wa Tanga, miradi ambayo ipo katika ushoroba wa barabara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayoanzia Lungalunga huku utekelezaji wake ukiwa unaendelea.


Barabara hiyo inaanzia Lungalunga nchini Kenya kupitia mpaka wa Horohoro (mpaka wa Tanzania na Kenya) kuelekea Pangani mkoani Tanga kwenda Hifadhi ya Taifa ya Saadan hadi Makurunge-Bagamoyo mkoani Pwani.



Hayo yamesemwa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga, Mhandisi Danstan Singano ambapo amesema, ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa upande wa Tanzania umegawanywa katika sehemu nne.



Mhandisi Singano ameitaja sehemu ya kwanza ya ujenzi wa barabara hiyo kuwa ni barabara ya kutoka Tanga hadi Pangani yenye urefu wa Km 50 ambapo ujenzi wa sehemu hiyo utatekelezwa kwa kutumia fedha za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa gharama ya shilingi Bilioni 77.


Amefafanua kuwa, sehemu ya pili ya mradi huo mkubwa ni ujenzi wa daraja la Pangani na barabara unganishi, mradi ambao umepata ufadhili kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

 

Kwa upande wake, Mhandisi wa mradi wa ujenzi wa daraja la Pangani Mhandisi Julius Msofe amesema, daraja jipya la Pangani litakuwa na urefu wa mita 525 na upana wa mita 13.5 ambapo katika upana wa mita hizo 13.5, mita 8 ni upana wa eneo la barabara (carriage way), mita 2 kila upande ni eneo la watembea kwa miguu na mita 1.5 ni kingo za daraja.


Mhandisi Msofe amefafanua kwa kusema kuwa, pamoja na ujenzi wa daraja hilo la Pangani, pia inahusisha na ujenzi wa barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 25.6.




"Pamoja na ujenzi wa daraja hili la Pangani, pia inahusisha na ujenzi wa barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 25.6 ambazo zimegawanyika sehemu tatu, barabara unganishi ya daraja yenye urefu wa kilometa 14.3, barabara za Pangani mjini zenye urefu wa kilometa 5.4  na barabara unganishi inayolekea eneo la Ushongo yenye urefu wa Kilometa 5.9" alisema Mhandisi Msofe na kuongeza kuwa




"Mradi wa ujenzi wa daraja la Pangani umefikia asilimia 32.16 , mradi huu umeanza kutekelezwa tarehe 07 Desemba mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika tarehe 06 Desemba, 2025. Mkandarasi anayetekeleza mradi huu anaitwa Shandong Luqiao Group

kutoka nchini China kwa gharama ya Shilingi Bilioni 82.4 Mhandisi Mshauri ni Lea Associates kutoka India.


Naye Nasri Abdul, ambaye ni mfanyakazi kutoka kampuni ya Shandong Luqiao Group akiongea kwa niaba ya wafanyakazi wenzake amesema, Mbali na faida za kifedha wanazopata na kutumia kwa ajili ya kujikimu, kuhudumia familia pamoja na kukidhi mahitaji mbalimbali ikiwemo ada za wanafunzi lakini pia wanavuna ujuzi na stadi mbalimbali ambazo hapo awali hawakuwa nazo.

Vile vile wafanyakazi hao wametoa shukran zao kwa viongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea mradi huo ambao umekuwa na faida kubwa sana kwao huku wakiahidi kuwa walinzi wa kwanza wa vifaa na mitambo inayotumika katika utekelezaji wa miradi hiyo.

 

Kukamilika kwa barabara ya Afrika Mashariki ambayo inaanzia Lungalunga nchini Kenya kupitia mpaka wa Horohoro (mpaka wa Tanzania na Kenya) kuelekea Pangani mkoani Tanga kwenda Hifadhi ya Saadan hadi Makurunge-Bagamoyo mkoani Pwani kutarahisisha na kuchochea shughuli za kiuchumi ikiwemo utalii, uchumi wa buluu, kurahisisha usafirishaji wa mazao ya biashara na kilimo kama vile Mkonge na Nazi na vile vile kupunguza muda wa usafiri ambao wananchi walikuwa wanautumia kutoka mkoani Tanga kwenda Dar es Salaam.