News

WAHUJUMU WA MIUNDOMBINU YA BARABARA KUSHUGHULIKIWA

Serikali imesema haitamvumilia mwananchi yoyote atakaebainika
kununua vyuma vyenye alama za barabara kama chuma chakavu, ili iwe fundisho kwa wahujumu wa miundombinu ya barabara.

Kauli hiyo imetolewa mkoani Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias Kwandika, mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2017-2018 kutoka kwa uongozi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), na kusisitiza kuwa anayeuza na kununua alama hizo sheria kali zitachukuliwa dhidi yake.

"Haiwezekani alama za barabarani zichukuliwe na kuuzwa na sisi tupo tunaangalia wakati sheria zipo niwape taarifa wafanyabiashara wanaonunua vyuma hivyo waache maramoja, kwa sababu tutawakamata pale tutakapowabaini," amesisitiza Naibu Waziri Kwandika.

Naibu Waziri Kwandikwa ametumia rai hiyo kuwataka Wakala wa Barabara za Vijijini (TARURA) kupitia upya miradi ya barabara ili kuhakikisha matengenezo yanayofanyika yanakidhi viwango vinavyotakiwa.

Aidha, ameongeza kuwa Serikali inafahamu TARURA ina changamoto kubwa hivyo ni wakati sasa wa ujenzi wa barabara za vijijini na mijini utekelezwe kwa viwango kama barabara zinazounganisha mikoa na Wilaya.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Bodi hiyo, Mhandisi Rashid
Kalimbaga amesema kuwa utekelezaji wa miradi ya barabara umekuwa ukiongeza kila mwaka ikiwa ni jitihada za Serikali katika kuhakikisha uchumi wa viwanda unafikiwa.

Ameongeza kuwa Bodi itaendelea kusimamia na kufuatilia fedha zote zinazotolewa na mfuko huo kwa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na TARURA ili zielekezwe kwenye miradi husika ili adhma ya Serikali ya Awamu ya Tano iweze kufikiwa.

Hadi kufikia robo ya pili ya mwaka wa fedha 2017/18, makusanyo ya fedha za bodi hiyo yameongezeka kutoka bilioni 101 mwaka 2006/07 hadi bilioni 917 ambapo ongezeko hilo limechangiwa na usimamizi wa karibu unaofanywa na Bodi hiyo.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano