TANROADS WAANZA MAZOEZI YAKUJIANDAA NA MICHUANO NCHINI
Dar es Salaam
17 Agosti, 2024
Wachezaji wa michezo mbalimbali wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) wameanza mazoezi ya kujiandaa kwa michezo mbalimbali ikiwemo ya Shirikisho la Michezo kwa Taasisi za Umma na Makampuni Binafsi (SHIMMUTA), itakayofanyika mkoani Tanga mwezi Novemba.
Afisa Michezo wa TANROADS, Bw. Edwin Nseke amesema, mbali na kujiandaa na michezo hiyo, pia kikosi chao kinajiandaa kuunda timu ya Wizara ya Ujenzi itakayoshiriki kwenye michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI), itakayofanyika kuanzia tarehe 18 Septemba hadi Oktoba 5, 2024 mkoani Morogoro.
“Taasisi yetu ni miongoni mwa taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Ujenzi, hivyo maandalizi yetu ni pamoja na wachezaji wetu kuunda timu ya wizara yetu itakayoshiriki SHIMIWI kama zilivyo nyingine zinazoshiriki chini ya mwamvuli wa wizara zao, na tumeanza mazoezi kwa wachezaji wetu kila mkoa wanafanya hivyo, ili watakaochaguliwa kuunda timu hiyo wakawakilishe vema,” amesema Nseke.
Amesema tarehe 17 Agosti, 2024 wamecheza mechi za kirafiki kwa michezo ya netiboli na mpira wa miguu dhidi ya timu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), iliyofanyika kwenye uwanja wa TRA uliopo Kurasini jijini Dar es Salaam, ambapo wenyeji wameshinda magoli 8-2 katika mpira wa miguu na netiboli 45-44.
Hatahivyo, Nseke ametoa wito kwa watumishi kuweka jitihada katika ufanyaji wa mazoezi, kwani husaidia kuuweka mwili imara na pia kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza, ya shinikizo la damu na kisukari.
Kwa upande wake kocha mkuu wa timu ya Netiboli ya TANROADS, Bi. Salma Hussein amesema maandalizi yao yanalenga kutwaa ubingwa wa michezo ya SHIMMUTA 2024.
“Tumeanza maandalizi sasa na tunakikosi kipana chenye wachezaji wazoefu, hivyo tunatarajia mwaka huu ubingwa utakuwa wetu, hivyo walioushikilia watambue hilo,” amesisitiza Bi. Salma.
Nao Katibu Mkuu na Katibu Msaidizi wa TRA. Bw. Kamna Shomari na Bi. Esther Haule wameipongeza, TANROADS kwa ushirikiano waliouonesha wa kukubali kucheza mechi ya kirafiki, ambayo imetoa mwanga kwa maeneo ambayo watayaboresha kabla ya kuanza kwa michuano hiyo ya SHIMMUTA, ambayo kwa upande wa mpira wa miguu ndio mabingwa watetezi na katika netiboli walishika nafasi ya tatu.
“Wito wangu ni viongozi kuruhusu michezo mahala pa kazi na kuongeza bajeti ambazo zitawezesha timu kushiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali, maana inaumuhimu sana kwa watumishi,” amesema Bw. Shomari.