BENKI YA DUNIA KUFADHILI MIRADI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU ILIYOATHIRIWA NA EL-NINO NA KIMBUNGA HIDAYA MTWARA
Mtwara
18 Agosti, 2024
Mpango wa Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) ni kujenga upya barabara ya Mtwara - Mingoyo - Masasi yenye urefu wa Kilometa 200 kwa kiwango cha lami na hiyo ni kufuatia barabara hiyo kuisha muda wake na kuchakaa.
Benki ya Dunia kama mshirika muhimu wa maendeleo nchini, imejitolea kufadhili ujenzi wa barabara hiyo muhimu kwa ajili ya uchumi wa mkoa wa Mtwara kwa kuwa inatumika kusafirisha makaa ya mawe kutoka Songea kwenda katika Bandari ya Mtwara.
Hayo yamesemwa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Dotto Chacha kwenye ziara ya ujumbe wa Benki ya Dunia ulipotembelea na kukagua miradi ambayo imepata ufadhili wa benki hiyo.
Mhandisi Dotto ameitaja miradi mingine inayofadhiliwa na Benki ya Dunia katika mkoa wa Mtwara kuwa ni pamoja na ujenzi wa madaraja matatu ya Lukuledi ,Maparawe na Njawala ambapo yatajengwa madaraja mapya huku mengine yakiongezewa uwezo.
Mha. Chacha amesema kuwa, ujenzi wa barabara ya kutoka Mtwara – Mingoyo - Masasi kwa kiwango cha lami utahusisha uwekaji wa miundombinu ya taa za barabarani pamoja na upanuzi barabara hiyo.
"Mpango wa serikali ni kuweka wakandarasi wawili na kujenga mizani miwili ya kisasa ili kurahisisha magari yanayosafirisha makaa ya mawe na bidhaa mbalimbali kupimwa haraka bila kuchelewa.," amesema Mha Dotto.