News

MRADI WA LUTUKIRA – SONGEA WAUFIKISHA UJUMBE WA BENKI YA DUNIA MKOANI RUVUMA

MRADI WA LUTUKIRA – SONGEA WAUFIKISHA UJUMBE WA BENKI YA DUNIA MKOANI RUVUMA

 

Songea

15 Agosti, 2024

Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inayonufaika na ufadhili wa Benki ya Dunia katika miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara na madaraja kupitia mradi wa Ushirikiano wa Usafiri Tanzania (TanTIP).


 

Kupitia Mradi wa TanTIP, Mkoa wa Ruvuma utanufaika kupitia ujenzi wa barabara ya kutoka Lutukira hadi Songea pamoja na barabara ya mchepuko ya Songea (Songea Bypass) maarufu kama Ushoroba wa Mtwara (Mtwara Corridor) yenye jumla ya urefu wa Kilometa 116 kwa kiwango cha lami.




Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Rubara Marando kwenye ziara ya ujumbe wa Benki ya Dunia uliotembelea na kukagua miradi wanayoifadhili mkoani humo.




Mha. Marando ameongeza kuwa, kitendo cha Benki ya Dunia kukubali kufadhili miradi ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, madaraja, viwanja vya ndege nchini kunatokana na mchango na msukumo wa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza na kuimarisha mahusiano mazuri na wadau pamoja na washirika wa maendeleo.




"Mahusiano yetu mazuri na washirika wetu wa Maendeleo yamewezesha wadau hawa (World Bank) kupokea mapendekezo ya miradi yetu na kuifadhili, na tunaishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada ambazo inaendelea kuzifanya kwa lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi. Wake," amesema Mha. Marando.



Kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Lutukira hadi Songea pamoja na barabara ya mchepuko ya Songea (Songea Bypass) kutarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa abiria na bidhaa, kuchochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla pamoja na kupunguza ajali  zinazotokea mara kwa mara.