News

WATAALAM WA MAZINGIRA WA TANROADS WAFANYA TATHMINI YA MIRADI YA MIUNDOMBINU YA MKOA WA MANYARA

WATAALAM WA MAZINGIRA WA TANROADS WAFANYA TATHMINI YA MIRADI YA MIUNDOMBINU YA MKOA WA MANYARA

 

Manyara

14 Agosti, 2024

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Manyara inaendelea na kazi ya kufanya tathimini ya mazingira katika miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja katika mkoa huo, ambapo kazi hiyo inafanywa na wataalamu kutoka kitengo cha mazingira cha Makao Makuu na wa ofisi ya TANROADS Mkoa wa Manyara.


Wataalamu hao wametembelea ofisi za Wakala ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), kwa lengo la kufanya tathmini ya mazingira ikiwa ni sehemu ya kuangalia namna mvua kubwa zilizonyesha kuanzia mwaka 2023 hadi mwezi Aprili mwaka 2024 huu zilivyoathiri miundombinu ya maji na ikizingatiwa kuwa miradi ya ujenzi wa barabara katika Mkoa wa Manyara ina mabomba ya maji ya RUWASA.




Meneja wa RUWASA Mkoa wa Manyara, Mhandisi Wolta Kirita amewashauri wataalamu hao wa TANROADS kutumia maji ya bomba lililoko eneo la Minjingu ili kumrahisishia mkandarasi kazi wakati wa ujenzi wa daraja hilo.




Vilevile wataalamu hao wametembelea eneo la kijiji cha Dabil kata ya Dabil, ambalo linatarajiwa kujengwa daraja ili kuwaondolea adha ya kuathiriwa na mvua zenye kusababisha maporomoko ya mawe katika eneo hilo.



Kwa upande wao, wananchi wa Dabil wamewashukuru wataalamu hao kwa ujenzi wa daraja hilo, litakalowasaidia kupita wakati wanapokwenda kwenye mashamba yao, ambayo awali yalikuwa yakiharibiwa na maporomoko ya maji na mawe.


Pia wataalamu wa mazingira wametembelea eneo la Katesh linalotarajiwa kujengwa daraja, baada ya lile la awali kuharibiwa na maporomoko ya udongo yaliyotokea mwezi Desemba mwaka jana.

Kwa upande wa wananchi wa eneo hilo la Kateshi wameishukuru TANROADS kwa kufanya jitihada ya kuboresha miundombinu katika eneo hilo na kuahidi kuwapa ushirikiano pindi mradi huo utakapoanza.