News

BILIONI 146 KUTUMIKA MATENGENEZO YA DHARURA UJENZI WA MADARAJA MKOANI LINDI

BILIONI 146 KUTUMIKA MATENGENEZO YA DHARURA UJENZI WA MADARAJA MKOANI LINDI

 

Lindi

15 Agosti, 2024

Kuanzia mwezi OKtoba, 2023 hadi kufikia Mei, 2024 Tanzania ilikumbwa na kadhia ya mvua kubwa za El-Nino pamoja na Kimbunga Hidaya iliyoathiri hali ya hewa nchini na kusababisha athari hasi kwa wananchi kukosa makazi, vifo, magonjwa ya milipuko, uharibifu wa miundombinu ya barabara pamoja na madaraja.

 

Katika eneo la miundombinu ya barabara za Mkoa wa Lindi ziliathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na madhara ya mvua hizo zilizonyesha mfululizo ambapo hata hivyo Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan ikatoa fedha jumla ya Shilingi Bilioni 19 za Kitanzania kwa ajili ya matengenezo ya dharura na kurejesha mawasiliano kwa haraka.

 

Akizungumzia Ofisi kwake Mkoani Lindi, Msimamizi wa Kitengo cha Mipango wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS),  Mhandisi Jastas Mpenihaka amesema kuwa kiasi cha Shilingi Bilioni 13 zimetumika kwa ajili ya matengenezo ya dharura kwa kujaza mawe, vifusi na kuweka makalavati ya plastiki katika barabara kuu katika maeneo mbalimbali ya Somanga Mtama, Kipwata, Mikereng’ende, Matandu, Lingaula, Mbanga na Mbwemkuru.

 

Amesema kiasi cha Shilingi Bilioni 6 zimetumika kwa ajili ya matengenezo ya dharura kwa kujaza mawe, vifusi na kuweka makalavati ya plastiki katika baadhi barabara Mkoa kwa barabara ya Nangurukuru – Liwale, Liwale – Nachingwea na Tingi – Kipatimu.

 

Naye, Msimamizi wa Kitengo cha Miradi ya Maendeleo TANROADS Mkoani Lindi, Mhandisi Fred Sanga amesema kuwa mvua za El-Nino pamoja na kimbunga Hidaya ziliathiri maeneo mengi katika barabara za mkoa wa Lindi, ambapo athari kubwa zaidi ilikuwa katika barabara za mikoa na barabara kuu hususani maeneo ya Somanga-Mtama, Mikereng’ende, Mbwemkulu, na Kipwata.

 

Amesema, kwa kuwa matengenezo hayo ya dharura yalikuwa ni suluhisho la muda mfupi kwa ajili ya kurejesha mawasiliano; Serikali inaendelea na mkakati kabambe wa suluhisho la kudumu kupitia mdau wa maendeleo Benki ya Dunia wa kujenga madaraja katika maeneo yote yaliyoathiriwa na mvua hizo za El-nino na kimbunga Hidaya.