BARABARA YA SENGEREMA - NYEHUNGE KM 54.5 KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI
Mwanza
14 Agosti, 2024
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema taratibu za kumpata mkandarasi mwingine ziko katika hatua za mwisho ili kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Sengerema-Nyehunge Km 54.5 mkoani Mwanza.
Akizungumza katika ziara ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Sengerema mkoani Mwanza, Naibu Waziri Mha. Kasekenya amesema zaidi ya shilingi Bilioni 73 zinatarajiwa kutumika kwenye ujenzi huo, ili kuyaunganisha kwa barabara ya lami majimbo ya Sengerema na Buchosa na hivyo kuchochea shughuli za uvuvi, kilimo na biashara mkoani Mwanza.
Aidha Mha. Kasekenya amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya Sengerema-Kamanga Km.32 kwenye wilayani Sengerema, ambayo ujenzi wake unafanyika kwa awamu.
Pamoja na ujenzi wa barabara Serikali pia inajenga kivuko cha Buyagu-Mbarika ambacho ujenzi wake umefikia asilimia 55 ili kuunganisha wilaya za Sengerema na Misungwi na ujenzi wa kivuko kipya cha Kome-Maisome kitakachokuwa na uwezo wa kubeba tani 170 na magari 22 na hivyo kupunguza adha ya usafiri wilayani Sengerema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ameipongeza Wizara ya ujenzi kwa kasi ya ujenzi wa daraja la J.P Magufuli Kigongo-Busisi lenye urefu wa Km 3 na barabara unganishi Km 1.6, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuweka alama zote za tahadhari katika daraja hilo kubwa nchini pindi litakapokamilika.
Amesisitiza umuhimu wa Wizara kuimarisha uwezo wa kuwapima vizuri wakandarasi kabla ya kuwapa mikataba ya miradi ili kuharakisha ujenzi wa miundombinu.
"Hakikisheni mnapata wakandarasi makini ili miradi ijengwe kwa wakati na ubora na hivyo kuleta tija kwa wananchi", amesisitiza Balozi, Dkt. Nchimbi.