RAIS SAMIA AFUNGUA BARABARA YA SUMBAWANGA – MATAI – KASANGA
Sumbawanga
16 Julai, 2024
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefungua barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga Port (Km 107.14) wilayani kalambo mkoani Rukwa.
Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan, amefungua barabara hiyo leo tarehe 16 Julai 2024, ambapo katika ufunguzi huo amewataka wananchi kuitunza barabara hiyo kwa manufaa ya kızazi kijacho.
“Niwaombe Wananchi na Kalambo na wasafirishaji wote kutunza miundombinu ya barabara, kwa kuacha kulima au kufukua fukua pembezoni mwa barabara kwani kufanya hivyo kunasababisha kuharibika kwa haraka kwa barabara zetu,” amesema Dkt Samia Suluhu Hassan.
Vile vile, amesema kufungua kwa barabara hiyo kutarahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao na mifugo kutoka Mkoa wa Rukwa kwenda mikoa mingine na nchi jirani kama Rwanda, DRC na Burundi na kutaongeza uchumi wa nchi.
“Tunaenda kukuza uchumi wa biashara kati yetu na nchi jirani, na wananchi wa Kalambo ni wakulima wazuri sana, sasa mtapata urahisi wa kusafirisha na sio Kalambo peke yake, mazao yatakayolimwa ndani ya Mkoa wa Rukwa na Katavi yatapata urahisi wa kusafirishwa,”amesema Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Pia, ametoa wito kwa wananchi wa Kalambo na wasafirishaji nchi nzima, kutunza miundombinu ya Blbarabara ili idumu kwa muda mrefu kwani ujenzi wa barabara ni gharama kubwa hivyo zitunzwe.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amesema miradi ya barabara iliyokamilika katika Mkoa wa Rukwa ni pamoja na barabara ya Sumbawanga – Matai – Kasanga Port (km 107.14),Tunduma – Sumbawanga (km 220), na Sumbwanga - Kanazi – Kizi – Kibaoni (km 151.6) kwa kiwango cha lami.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema ujenzi wa sehemu hii ya barabara ni muendelezo wa juhudi za serikali za kujenga ushoroba huu kwa kiwango cha lami ambapo hadi sasa jumla ya kilometa 802.55 kati ya kilometa 1,286 zimeshajengwa na kukamilika ambazo ni sawa na asilimia 62.40.