“SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA MTANDAO WA BARABARA MKOANI SONGWE”
Songwe
18 Juni, 2024
Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Songwe inaendelea na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwa ni pamoja na kuboresha mtandao wa barabara, kujenga eneo maalum la maegesho ya magari, ujenzi wa sehemu ya kugeuzia magari (Turning Point) na mizani za kupima uzito wa magari.
Akizungumza na Kipindi cha TANROADS Mkoa kwa Mkoa hivi karibuni, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe Mha. Suleiman Bishanga amesema serikali inaboresha miundombinu ya barabara ya Tunduma kwenda Igawa kwa kujenga mizani mbili katika Kijiji cha Iboya ambapo zaidi ya mita 800 kwa Kilomita 2.5 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
“Mbele yake tunajenga eneo la maegesho ya magari (Parking) ile parking haina uhusiano na ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja wa magari cha Iboya maana wananchi wanaulizia je ile parking inayojengwa Chimbuya ndio iliyotakiwa kujengwa Iboya?, mpango wa serikali ni kupunguza msongamano wa magari barabarani ile ya Chimbuya inajengwa kwa ajili ya kusaidia kupunguza foleni kwa magari ambayo yanaelekea Tunduma baada ya kuwa yamepima Iboya kwa hiyo ni parking mbili tofauti na zote serikali inazitekeleza’’ amesema Mha. Bishanga na kuongeza:
“Kwa upande wa Tunduma kule tumeenda kujenga Turning Point, sehemu ambayo magari yatakwenda kuzunguka na kurudi, magari yakifika Tunduma yanaenda kama kilomita 6 kutoka pale yanakwenda kugeuza kwa ajili ya kuja kuingia kwenye border ya Zambia, serikali ilitoa fedha ili kuwarahisishia wasafirishaji wasipate adha kwenye kugeuza magari, pale tutatengeneza round about nzuri kwenda mpakani Tunduma’’ ameeleza.
Wakizungumzia ujenzi wa maegesho hayo ya magari; madereva wanaotumia barabara hiyo akiwemo bwana Raphi Msomari na Zidadi Omari wameishukuru serikali na kusema kuwa “tunaamini parking hii itakuwa bora sana kwa sababu huduma zote za kijamii ikiwemo vyoo na maji vitakuwepo tofauti na maeneo mengine ambayo hayana huduma hizo na ulinzi ni mdogo’’
Wameongeza kuwa “tunaimani Serikali ikishaweka parking hapa usalama utakuwepo, vyombo vyetu vitakuwa salama na sisi wenyewe tutakuwa salama na huduma zitakuwa nzuri’’