MAANDALIZI YA UJENZI WA BARABARA YA HOLILI-TAREKEA YAKAMILIKA
Dodoma
13 Juni, 2024
Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha maandalizi ya nyaraka za zabuni kwa ajili ya kumpata Mkandarasi wa ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara ya Tarakea - Holili yenye urefu wa Kilometa 52.8 ambapo itaanza na sehemu ya kilometa 10 kuanzia kijiji cha Munga hadi kijiji cha Kiwanda na sehemu iliyobaki serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi.
Hayo yameelezwa leo tarehe 13 Juni, 2024 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi Mha. Godfrey Kasekenya wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Zuwena Bushiri aliyeuliza ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa barabara ya Holili - Tarakea wilaya ya Rombo.
"Kutokana na changamoto ya barabara ya Rombo kuwa na msongamano wa malori, miinuko na kona kali, ndio maana Serikali imekuja na mpango wa kujenga barabara kutoka Holili hadi Tarakea na tumeshakamilisha usanifu kwa barabara yote na tumeshatangaza kuijenga kwa kiwango cha lami kwa kuanza na kilometa 10", amesema Mha. Kasekenya.
Aidha Mha. Kasekenya amesema barabara ya Kibiti - Mloka yenye urefu wa kilometa 100.18 imeingizwa kwenye mpango wa mwaka wa fedha 2024/25 kwa ajili ya kuifanyia usanifu na upembuzi wa kina na ukikamilika serikali itatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami.
Kasekenya amesema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kibiti Twaha Mpembenwe aliyeuliza Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya Kibiti - Dimani - Mloka kwa kiwango cha lami.
"Mheshimiwa Mbunge anafahamu hii barabara ipo kwenye ilani na mwakani tunataraji kuifanyia usanifu na upembuzi wa kina na hii barabara ndio inatumika kwa sasa na wenzetu wa TANESCO kupeleka vifaa vya umeme kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere kwa hiyo tutatimiza azma ya Serikali ya kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami", amesisitiza Mha. Kasekenya.