SERIKALI KUJENGA KWA KIWANGO CHA LAMI BARABARA ZINAZOUNGANISHA RELI YA SGR
Dodona
10 Juni, 2024
Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imesema ipo katika hatua mbalimbali za kujenga kwa kiwango cha lami barabara zote zinazounganisha stesheni za Reli ya SGR, kwa sasa wameanza na stesheni zote za kutoka mkoa wa Dar es Salaam hadi Dodoma ambapo ujenzi wa Reli ya SGR uko katika hatua za mwisho.
Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma leo tarehe 10 Juni, 2024 na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya wakati akijibu swali la Mbunge wa Kibaha Vijijini, Mheshimiwa Michael Constantino Mwakamo, aliyeuliza Serikali haioni umuhimu wa ujenzi wa vipande vya barabara za lami kuunganisha Barabara Kuu na Reli ya SGR kwa lengo la kurahisisha wasafiri kufika Stesheni.
“Niwahakikishie kuwa barabara zote zinazokwenda kwenye stesheni za SGR ni suala ambalo linatakiwa lifanyike haraka sana ili tusiwakwamishe wananchi watakaotoka kwenye barabara kuelekea kwenye vituo vya SGR”, amesisitiza Kasekenya.
Aidha ameeleza kuwa kwa upande wa Mkoa wa Pwani, taratibu za manunuzi ya ujenzi wa barabara ya Mlandizi – Ruvu Stesheni SGR (km 22) ziko hatua za mwisho.