MPANGOKAZI WA TANROADS, ZANROADS KUANZA KUTUMIKA MWAKA 2024/25
Dodoma
08 Juni, 2024
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara Zanzibar (ZANROADS) wameweka mpangokazi wa kipindi cha mwaka mmoja, ambao utekelezaji wake utaanza kutumika rasmi kwenye mwaka wa fedha 2024/25.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta amesema leo tarehe 08 Juni, 2024 Jijini Dodoma katika kikao cha uwasilishaji wa mpangokazi wa utekelezaji wa Hati ya mashirikiano kati ya TANROADS na ZANROADS uliofanywa na Kamati ya Wataalam amesema mpangokazi huo utaanza kufanya kazi rasmi baada ya kusainiwa na uongozi wa juu wa pande zote mbili.
Mha. Besta amesema kuwa mpangokazi huo ni wa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2024/25 hadi 2028/29 ambapo utakuwa unahuishwa kila mwaka, lakini kwa mwaka ujao wa fedha wataanza na vipengele vinne vya kuanzia kazi, ambavyo vimeainishwa kwenye rasimu hiyo, ambavyo ni kuandaa na kuendesha mafunzo, semina na warsha kwa ajili ya kujenga uelewa juu ya miongozo mbalimbali ya uendeshaji na usimamizi katika shughuli za ujenzi wa barabara. Ushiriki wa pamoja na kubadilishana Wataalam katika kazi kwenye maeneo ya mradi.
Amesema vipengele vingine ni pamoja na kuandaa na kuendesha vikao kazi vya kuandaa miongozo na taratibu za usimamizi na uendeshaji wa mizani, pia kuandaa mafunzo ya namna ya uendeshaji na utunzaji wa mizani kwa watumishi wa ZANROADS; na kutoa elimu kwa wadau wa usafirishaji kuhusu uanzishwaji na uendeshaji wa shughuli za mizani na umuhimu wake.
Mha. Besta amesema vipengele vingine ambavyo vitatekelezwa kwa kuanzia robo ya kwanza hadi ya nne ya mwaka wa fedha 2024/25 ni pamoja na kuandaa nyaraka za uanzishwaji wa kitengo cha Ushauri Elekezi Zanzibar (ZANROADS Engineering Consulting Unit - ZECU); kuandaa na kuifanya ziara za mafunzo na kubadilishana uzoefu; Ufuatiliaji wa maendeleo ya uanzishwaji wa kitengo cha ZECU na kuratibu shughuli za kijamii ikiwemo mashindano na michezo mbalimbali kati ya taasisi hizi.
“Tunaamini utekelezaji wa mpangokazi huu kutasaidia kuimarisha uwezo wa utendaji wa taasisi zetu hizi, sisi tunalakujifunza kwa wenzetu na wao wanalo la kujifunza kutoka kwetu,” amesema Mha. Besta.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa ZANROADS, Mha. Cosmas Masolwa amesema kutokana na mashirikiano haya yataendelea kuleta na kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi hizi mbili.
“Ushirikiano huu naamini utadumu la pande zote mbili kila mmoja atanufaika kutokana na jambo jipya kutoka kwa mwenzake, ukiangalia wenzetu wapo mbele mfano sisi hatuna mzani wa magari huku kwetu Zanzibar na sasa mahoteli makubwa makubwa yanajengwa na magari mengi yanayoleta malighafi ya ujenzi yanakuja na mawe, mchanga hivyo ni rahisi kuharibu barabara zetu, hivyo tunaamini tutajifunza kutoka kwa wenzetu,” amesema Mha. Masolwa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya ZANROADS, Msanifu Majengo Yasser de Costa amepongeza mashirikiano haya yaliyochagizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi na anaamini yatafanikiwa kunilingana na utekelezaji wa vipengele vilivyopo kwenye kila mwaka wa utekelezaji.