News

TANROADS YAFANYA USAFI WA MAZINGIRA MACHINGA COMPLEX YA DODOMA

TANROADS YAFANYA USAFI WA MAZINGIRA MACHINGA COMPLEX YA DODOMA

Dodoma

04 Juni, 2024

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), imesisitizia wananchi kufanya usafi mara kwa mara kwenye maeneo yanayozunguka barabara na kuacha kutupa takataka ndani ya madaraja.

Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 4 Juni, 2024, Meneja wa Usimamizi wa Mazingira na Jamii, Bi. Zafarani Madayi wakati wa kufanya usafi wa mazingira katika eneo la kuanzia Kiwanja cha Ndege mpaka soko la Wamachinga, ikiwa ni Maadhimisho ya Wiki ya Maizngira Duniani yanayofanyika Jijini Dodoma.

Bi. Madayi amesema uchafu ndani ya madaraja unasababisha mafuriko baada ya maji kushindwa kupita vizuri na kupoteza mwelekeo na kuchimba barabara na kuharibu makazi ya wananchi waliokaribu..

“Tusaidiane watanzania wote iwe mjini au vijijini tushirikiane kwa kutoweka na kutupa uchafu barabarani na kwenye makalvati, ili fedha hizi zitakazotumika kwa ajili ya matengenezo basi zitumike kwa kujengea miundombinu mipya,” amesema Bi. Madayi.

Amesema usafi huo umezingatia uondoaji wa michanga pembezoni mwa barabara, kuondoa uchafu chini ya kalvati, mifereji na kulima nyasi kuzunguka barabara, ambapo uchafu ukiachwa unaleta madhara kipindi cha mvua kwa kwenda kuziba makalvati.

“Tumeshirikiana na wakazi na wenyeji wa hapa pamoja na wakandarasi katika kufanya usafi barabarani na maeneo ya kwenye makaravati, maana ni muhimu sana kwa sababu inasaidia barabara kudumu, bila kuathiriwa na maji na tutambue kutunza mazingira ni jukumu letu sote na sio la TANROADS pekee,” amesema Bi. Madayi.

Amesema kuwa mbali na uharibifu wa barabara unaotokana na mafuriko, pia kumekuwa na athari kwa binadamu kwa kuleta magonjwa ya maambukizi kama kipindupindu na kuhara, ambayo hudhoofisha nguvu kazi ya taifa.
Halikadhalika amewataka wakandari wenye majukumu ya kufanya ukarabati na usafi kwenye barabara, makalvati, madaraja, na mifereji, kutimiza wajibu wao ili kuweka mazingira hayo salama bila kuathiriwa na mafuriko, kwa kuwa wanalipwa fedha nyingi kwa ajili ya mojawapo ya kazi hizo.

Naye mkazi wa Ihumwa, Dodoma, Juma Kimaro amesema wananchi wajitahidi kuweka mazingira yao katika hali ya usafi, ili kuyaweka katika hali ya usafi.