News

DKT. BITEKO AIPONGEZA TANROADS KWA KAZI NZURI

DKT. BITEKO AIPONGEZA TANROADS KWA KAZI NZURI


Dodoma;

03 Juni, 2024

 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mh. Dkt. Dotto Biteko ameipongeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege.

Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo leo tarehe 3 Juni, 2024 wakati alipotembelea banda la maonesho la TANROADS kwenye ufunguzi wa maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani, yanayofanyika katika viwanja vya ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete,jijini Dodoma.

Dkt. Biteko alikuwa mgeni rasmi wa ufunguzi wa Maadhimisho haya muhimu kwenye ukuaji wa sekta ya mazingira nchini, ambapo kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni:”Urejeshwaji wa ardhi na usahimilivu wa hali ya jangwa na ukame”.

“Hongereni sana tumeona namna mlivyofanya wakati wa bajeti mlitoa maelezo mengi mazuri, nawapongeza sana na kwa leo sina swali na kama nitakuwa nalo nitawatumia kwa njia ya mtandao” Alisema Dkt. Biteko

Awali akitoa maelezo mbalimbali Meneja wa Usimamizi wa Mazingira na Kijamii wa TANROADS, Bi. Zafarani Madayi alimweleza Naibu Waziri Mkuu namna wakala hiyo inavyotunza mazingira kwa kurejeshea ardhi uhalisia wa awali mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege.

Bi. Madayi alisema kuwa wakati wa ujenzi wa miundombinu hiyo, kumekuwa na uchimbaji wa malighafi za ujenzi ukiwemo mchanga, mawe na kokoto kwenye maeneo mbalimbali na hulazimika kurudishia hali yake ya awali kwa kupanda miti na nyasi za asili.

Katika hotuba yake, Dkt Biteko amesisitiza kuwa mazingira kuwa sio kupanda mti pekee bali mazingira ni kila kitu mfano ukiweka nguzo ya umeme unaokwenda kwa wananchi hiyo ni sehemu ya mazingira, hakikadhalika wanaojenga barabara nao ni sehemu ya mazingira.

Amesema hakuna yeyote anaweza kufanya jambo lolote bila kuhusisha mazingira aidha kuyatunza au kuyaharibu kwa namna yeyote.

“Kupanda mti ni jambo moja na kulinda na kuutunza mti ni jambo jingine tena la gharama sana, hivyo itakuwa haina maana yeyote tukishindwa kuzungumza ili tujue wizara gani haijafika ili itambuliwe,” amesema Dkt. Biteko