WATAALAM WALIOSTAAFU KUENDELEA KUTUMIKA KATIKA UJENZI NA MATENGENEZO YA BARABARA- BASHUNGWA
Dodoma
29 Mei, 2024
Wizara ya Ujenzi kupitia taasisi zake Bodi ya Wakandarasi (ERB) na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inaandaa utaratibu wa kutumia wataalam wa ndani waliostaafu katika ujenzi na matengenezo ya barabara.
Haya yamebainishwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa wakati wa kuwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25, Bungeni jijini Dodoma leo, Mei 29, 2024
Amesema hatua hiyo ni katika kujenga uwezo wa ndani ya taasisi na wastaafu wabobezi katika usimamizi wa miradi badala ya kutegemea wataalam nje.
“Tumeanza utaratibu wa kutumia wataalam wa ndani waliostaafu yaani retired but not tired katika ujenzi na matengenezo ya barabara.”
Amesema Kitengo cha ndani cha Ushauri wa Kihandisi cha TANROADS (TECU) kinaendelea kuwatumia wahandisi wabobezi waliostaafu katika usanifu na usimamizi wa miradi.
“Hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza utegemezi wa wahandisi washauri kutoka nje. Jambo hili la kutumia wastaafu pia linatoa fursa kwa wataalam wanaochipukia na ngazi ya kati kujifunza kutoka kwa wastaafu wabobezi ambao wako nyumbani wakati ujuzi wao bado unahitajika katika ujenzi wa taifa letu.”
Amesema TANROADS inatumia TECU katika usanifu na usimamizi wa miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja.
“Hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za usimamizi wa miradi pamoja na muda unaotumiwa katika ununuzi wa wahandisi washauri,”
Amesema TECU imeshiriki kwa mafanikio katika utekelezaji wa miradi kadhaa ya kimkakati, ikiwemo mradi wa uzalishaji wa umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, mradi wa ujenzi wa barabara ya Njia nane (8) ya Kimara-Kibaha (Km. 19.2), mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Geita, na ujenzi wa kiwanda cha sukari cha Mbigiri.