News

MITAMBO YA KUPIMA UBORA WA BARABARA KULETA MAGEUZI: DKT. TULIA

MITAMBO YA KUPIMA UBORA WA BARABARA KULETA MAGEUZI: DKT. TULIA

Dodoma

27 Mei, 2024

SPIKA wa Bunge, Dkt. Tulia Akson ameisisitiza Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha miradi yote ya  barabara inayokamilika inapimwa ubora kwa kutumia vifaa maalum kabla ya Mkandarasi kuikabidhi kwa serikali.

 

Dkt Tulia amesema hayo leo tarehe 27 Mei 2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akifungua maonesho ya siku mbili ya Sekta ya Ujenzi, ambapo amempongeza Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye uwekezaji wa eneo la miundombinu ya barabara.

 

Amesema kuwa mitambo na vifaa vya kisasa iliyonunuliwa hivi karibuni na TANROADS itaisaidia serikali kuondokana na changamoto ya kukabidhiwa  miradi ya barabara iliyo chini ya kiwango.

 

Spika amesema kabla ya hapo kulikuwa na matumizi yasiyoridhishwa ya fedha za walipa kodi kwani baadhi ya makandarasi walikuwa wakikabidhi barabara halafu mvua zikinyesha kipindi kimoja zinaweka mashimo na kufanya wabunge kuanza kutafakari namna ya kuishauri kwamba imejengaje barabara.

 

Amesema tatizo halikuwa ujenzi bali ukosefu wa teknolojia ya kupima udongo tangu mwanzo wa kazi lakini kwa sasa hali hiyo haitajitokeza na kuomba wataalamu kutumia teknolojia hiyo kupokea miundombinu iliyokamilika.

 

Aidha, Dkt Tulia amesema kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Ujenzi imetimiza kile ambacho Watanzania wanakihitaji.

 

“Tunafahamu miaka miwili iliyopita Rais Samia alipewa tuzo maalum ya miundombinu kwenye eneo la barabara, tuzo hii bila shaka kwa maonesha haya inaonyesha namna ambavyo  tumepiga hatua kubwa kwenye suala la miundombinu,” amesema Dkt Tulia.

 

Kuhusu Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) amewapongeza kwa kufanya mageuzi ya kuwatafuta wateja waliko na kufanya kazi ya matengenezo kwa saa 24 kwa kutumia karakana zinazotembea (Mobile Workshop) kuliko ilivyokuwa ambapo walisubiri kupelekewa kazi za kufanya kwenye maeneo yao.

 

Amesema kwa namna Tanzania ilivyo kubwa, kuna haja ya kuwa na magari mengi ya Karakana zinazotembea na kuendelea kupokea ushauri unatolewa na Bunge ili waipatie Serikali mapato kutokana na utendaji kazi wao mzuri licha ya kuwa anatambua kuna changamoto nyingi katika Taasisi hiyo.

 

 

Awali,  Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa akimkaribisha Spika, amesema kumekuwa na mageuzi makubwa ndani ya Wizara hiyo kutokana na uwezeshwaji mkubwa wanaoupata kutoka kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

 

Bashungwa amesema wamejipanga ndani ya Wizara hiyo katika kuwahudumia Watanzania ili lengo la kiongozi mkuu wa nchi katika Sekta ya Ujenzi liweze kutimia.