SERIKALI KUENDELEA KUIJENGA BARABARA YA RUJEWA-MADIBIRA-MAFINGA KM 151.1 KWA AWAMU
Dodoma
23 Mei, 2024
Serikali imesema itaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Rujewa –Madibira hadi Mafinga yenye urefu wa kilometa 151.1 ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na maendeleo wilayani Mbarali mkoani Mbeya.
Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya ameyasema hayo leo tarehe 23 Mei, 2024, bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mbarali na kusisitiza kuwa nia ya serikali ni kuhakikisha inakamilisha ujenzi huo kadri ya upatikanaji wa fedha
“Mh.Spika nikuhakikishie adhma ya Serikali ni kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ili kuleta maendeleo kwa wananchi wa wilaya ya Mbarali ambao eneo lao lina uzalishaji mkubwa wa mazao na hivyo kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla,”Amesema Kasekenya.
Aidha amesema taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata Mkandarasi wa ujenzi kwa sehemu ya Igoma hadi Kinanyambo ‘A’ yenye urefu wa Km 52.2 zinaendelea ambapo mkataba unatarajiwa kusainiwa mwishoni wa mwezi Juni 2024.
Mh. Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Bahati Ndingo alitaka kujua ni lini serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Rujewa-Madibira hadi Mafinga kwa kiwango cha lami.