News

TANROADS MANYARA YAANZA KUTEKELEZA MAELEKEZO YA WAZIRI BASHUNGWA ENEO LA KATESH

TANROADS MANYARA YAANZA KUTEKELEZA MAELEKEZO YA WAZIRI BASHUNGWA ENEO LA KATESH

 

Manyara

20 Mei, 2024

Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Manyara imeanza kutekeleza maagizo ya Waziri wa Ujenzi (Mb) Mhe. Innocent Lugha Bashungwa aliyoyatoa mnamo tarehe 06 Aprili, 2024 katika hafla ya utiaji saini wa ujenzi wa barabara ya Dareda Center – Dareda Mission (Km 7) kwa kiwango cha lami.

 

Katika hafla hiyo Mhe. Innocent Lugha Bashungwa aliielekeza TANROADS kurejesha hali ya miundombinu iliyoathirika kufuatia maporomoko ya tope eneo la Katesh katika wilaya ya Hanang’ kwa kujenga Barabara za Huduma (Service Roads), Kusimika taa za barabarani, Kuweka paving blocks pande zenye maduka, kujenga mitaro ya mawe na zege, kuweka vivuko vya watembea kwa miguu pamoja na ujenzi wa makalavati sita (6).

 

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa eneo la Katesh, Meneja wa Mkoa TANROADS Manyara Mha. Dutu Masele ameeleza kuwa Mradi huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Ujenzi Mhe Innocent Lugha Bashungwa katika kuhakikisha mji wa Katesh unarejeshwa katika hali nzuri baada ya kukumbwa na athari za El nino mwezi Desemba mwaka 2023.

 

Ameeleza kwamba, kazi ambazo zinaendelea kwa sasa ni pamoja na kujenga barabara za huduma kwa kiwango cha lami, kusimika taa za barabarani 80, kuweka vivuko vya zege kwa ajili ya watembea kwa miguu na kujenga mitaro ya mawe na zege.

 

Aidha, Meneja amewaelekeza wananchi wa eneo la Katesh kulinda samani za barabara zinazowekwa ili ziweze kudumu kwa muda mrefu na kuongeza usalama wa watumiaji wote wa barabara usiku na mchana.

 

Kwa upande wa wananchi ambao ni watumiaji wakubwa wa barabara hiyo, wameipongeza Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuwajengea barabara za huduma na kwa namna ambavyo Serikali imekua nao bega kwa bega tangu kutokea kwa majanga ya maporomoko yaliyotokana na kumomonyoka kwa Mlima Hanang’