News

"SERIKALI IMEKIIMARISHA KITENGO CHA UTAFITI NA MAENDELEO (RDU) KWA KUWAPATIA VIFAA VYA KISASA NA WATAALAM" -  MHA. MATAKA

"SERIKALI IMEKIIMARISHA KITENGO CHA UTAFITI NA MAENDELEO (RDU) KWA KUWAPATIA VIFAA VYA KISASA NA WATAALAM" -  MHA. MATAKA

Dar es Salaam

19 Mei, 2024

Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), imeimarisha Kitengo cha utafiti na Maendeleo (Research and Development Unit – RDU) kwa kukipatia vifaa vya kisasa na kuongeza wataalam Wahandisi hatua, ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza kwa ufanisi kwenye utendaji wa kazi.

 

Akizungumza katika kipindi maalum kilichoandaliwa na kitengo cha Habari na Uhusiano cha TANROADS; Mkuu wa Kitengo hicho Mha. Mussa O. Mataka ameishukuru serikali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzidi kuwezesha kituo hicho kwa kukipatia fedha za kununua vifaa vya kisasa ili kufanya kazi na kutimiza majukumu yake bila kukwama.

 

Ameeleza “kwa sasa hivi tunavifaa vingi ambavyo ni vya kisasa sana, tulifanya utafiti na tukaandaa mwongozo maalum kwa ajili ya usanifu wa lami baada ya kuanza kufanya kazi kwa kufuata ule mwongozo kwa kweli shida ile tuliyokuwa tunaiona ya kubonyea kwa lami zetu imepungua’’.

 

Amesema kwa sasa kitengo hicho kina sehemu kuu tatu ambazo ni Pavement materials inayoangazia zaidi barabara na usanifu, sehemu ya pili ni Testing and Quality Control inayosimamia kwa ujumla shughuli zote za upimaji na sehemu ya tatu ni Go Engineering inayoshughulika zaidi na utafiti wa udongo na miamba hasa kwa ajili ya majenzi ya barabara, madaraja majengo na hata mabwawa. 

 

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Barabara, Tafiti na Malighafi za Ujenzi, Mhandisi Mwandamizi John T. Malisa ameeleza umuhimu wa kufanya tafiti katika ujenzi ni pamoja na kusaidia kupata mbinu za kuboresha ufanisi wa barabara, usanifu na kupunguza kuharibika mapema (premature failures).

 

Amesema utafiti unahitajika kubadilisha teknolojia na ubunifu toka sehemu mbalimbali duniani ili ziweze kufaa katika mazingira yetu; akitolea mfano SUPERPAVE ya Marekani iliyobadilishwa kuwa SUPERPAVE ya Tanzania.

 

Ameongeza kuwa hayo yote yanalenga kupata miundombinu inayoendana na thamani ya fedha iliyowekwa, kusaidia kuokoa gharama za ujenzi wa barabara pamoja na kuiepusha serikali na hasara ambayo ingeweza kujitokeza iwapo barabara zitaharibika mapema.

 

Aidha Kwenye maabara Kitengo hicho kina vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na vile vyenye uwezo wa kupima na kubaini barabara itaishi miaka mingapi, uchakavu wake, itakuwa na uwezo gani; pamoja na gari yenye mtambo unaotumika kupima ubora wa barabara (ROAD DOCTOR SURVEY VAN), ambao unafanya kazi ya kunasua na kukusanya taarifa za barabara kwa ajili ya kuweza kupima ubora wake; taarifa hizo husaidia kuainisha maeneo salama na yenye changamoto yanayohitaji matengenezo.