TANROADS MANYARA YAENDELEA NA KAZI YA MATENGENEZO YA BARABARA YA NGARENARO-MBULU
Manyara
15 Mei, 2024
Serikali kupitia Wakala ya barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Manyara inafanya matengenezo ya Barabara ya Mkoa Ngarenaro (Babati) – Mbulu ambayo inaunganisha Makao Makuu ya Mkoa Babati na Wilaya ya Mbulu.
Hivi karibuni barabara hiyo iliathiriwa na maporomoko ya udongo kutoka katika milima ya Kiru eneo la Kiru Erri yaliyotokana na mvua kubwa ilionyesha katika Milima hiyo na kusababisha barabara hiyo kujifunga kwa muda.
Akizungumza baada ya kutembelea na kukagua eneo hilo leo tarehe 15 Mei 2024; Meneja wa TANROADS Mkoa wa Manyara Mhandisi Dutu Masele amesema, TANROADS inaendelea na kazi ya kufungua barabara hiyo kwa kutoa udongo ulioporomoka na kufunga barabara ambapo hadi sasa magari yameanza kupita upande mmoja wa barabara hiyo inayopita pembezoni mwa bonde la ufa.
Amesema ametoa wito kwa watumiaji wa barabara hiyo kuendelea kupita kwa tahadhari sehemu hizo zenye miinuko hasa kipindi hiki cha mvua kwani milima imejaa maji hivyo ni rahisi kutokea maporomoko kwenye maeneo hayo.
Mha. Masele ameeleza barabara hiyo ni muhimu Kiutawala kwani inaunganisha Wilaya ya Babati na Wilaya ya Mbulu, Kiuchumi inatumika katika shughuli za Usafirishaji wa mazao ya miwa yanayopelekwa katika viwanda vya uzalishaji sukari na pia kuyafikisha mjini kwenye masoko ya Manyara na Mikoa jirani.
Ameongeza kuwa timu ya Wahandisi kutoka TANROADS Manyara pamoja na Mkandarasi Job Engineering Ltd anayetekeleza kazi hiyo wapo katika eneo hilo ili kuhakikisha barabara inafunguka kwa haraka na inakuwa salama kwa watumiaji wa barabara wakati wote.