KAZI YA KUREJESHA MIUNDOMBINU YA BARABARA YA KIBAYA – KIBERASHI INAENDELEA
Manyara
10 Mei, 2024
Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Manyara inaendelea na kazi ya kurejesha miundombinu ya barabara eneo la Mbigiri na Pori kwa Pori katika Barabara ya Mkoa ya Kibaya hadi Kiberashi.
Barabara hiyo ilikumbwa na athari kubwa ya kusombwa kwa tuta la barabara kutokana na Mvua kubwa za El Nino zilizonyesha katika maeneo mengi ya Mkoa wa Manyara.
Hayo yameelezwa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Manyara Mha. Dutu Masele alipozungumza na kipindi cha TANROADS Mkoa kwa Mkoa leo tarehe 10 Mei 2024.
Ameeleza kuwa kazi zinazofanyika ni pamoja na kunyanyua tuta la barabara kwa wastani wa mita moja, kuweka tabaka la changarawe, kujenga vivuko vya maji (solid and vented drifts) pamoja na makalavati sita (6) ambapo hadi sasa kazi hiyo imefika asilimia 80.
Amesema barabara hiyo ni muhimu kwani inaunganisha Mkoa wa Manyara na Tanga katika Wilaya za Kiteto na Kilindi na inachochea uchumi kwa shughuli za Usafiri na Usafirishaji wa mazao kama vile mahindi na alizeti, ufugaji pamoja na usafirishaji wa malighafi za ujenzi ikiwemo gypsum inayotumika katika utengenezaji wa saruji (Cement).
Mha. Dutu ameongeza kuwa utekelezaji wa kazi hiyo unafanywa na Mkandarasi Mzawa, unasimamiwa na wataalamu wa ndani na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mwezi Mei 2024.