News

WAFANYAKAZI WA MIZANI KANDA YA ZIWA WAISHUKURU TANROADS KWA MAFUNZO ELEKEZI

WAFANYAKAZI WA MIZANI KANDA YA ZIWA WAISHUKURU TANROADS KWA MAFUNZO ELEKEZI

 

Mwanza

06 Mei, 2024

Wafanyakazi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kitengo cha mizani wa Kanda ya Ziwa wameshukuru kwa kupatiwa mafunzo elekezi ambayo yatawajengea uwezo na weledi mahala pa kazi.

 

Kwa nyakati tofauti wafanyakazi walioshiriki kwenye mafunzo hayo yenye lengo la kupata uelewa wa pamoja katika utekelezaji wa Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2018, taratibu za utendaji kazi kwenye mizani, maadili ya Utumishi wa Umma, elimu kuhusu vitendo vya rushwa na utoaji wa huduma bora kwa wateja wamesema wamefurahishwa nayo.

 

Bw. Kassim Jumanne, Afisa Mizani ya Usagara jijini Mwanza amesema mafunzo hayo yatawasaidia katika utendaji wao wa kazi wa kila siku kutokana na wasafirishaji kuongezeka kila siku.

 

“Tunashukuru kwa mafunzo haya maana yatatujengea uwezo wa kukabiliana na changamoto sehemu zetu za kazi, kutokana na uwingi wa magari mfano hapa mizani ya Usagara tunapina magari zaidi ya 1000 kwa saa 24,” amesema Jumanne.

 

Hatahivyo, amewaasa watumishi wenzake kuzingatia maadili ya kazi ili kulinda barabara zisiharibike na kuisaidia serikali kukua kwa uchumi kutokana na kuwa na barabara nzuri.

 

Naye Stella Matue, Afisa Mizani ya Bwanga mkoani Geita amesema mafunzo haya yatamsaidia kutoa elimu kwa wasafirishaji, ambao mara nyingi wamekuwa wakikiuka taratibu kwa kuzidisha uzito kwa kutokujua.

 

Kwa upande wake mhandisi Lumelezi Albert wa mizani ya Tinde mkoani Shinyanga, amesema mafunzo haya yatasaidia kuelimisha wasafirishaji namna gari inavyokutwa umezidisha mzigo, maana kwa sasa wengi hawaelewi wakidhani wanaonewa.

 

“Wasafirishaji wengi sio waelewa hasa gari inapokuwa imezidi uzito, kuna aina mbili za uzito wa kwenye ekseli za matairi ya gari na pili ni mzigo kuzidi katika uzito mzima wa gari yaani GVM, ambapo wanashindwa kutofautisha,” amesema Mha. Albert.

 

Hatahivyo, ameomba mafunzo haya yawe endelevu kwa kutolewe mara kwa mara ili kuwajengea uwezo, halikadhalika wasafirishaji nao wapewe mafunzo hayo waweze kujua sheria, kanuni na taratibu za mizani na mizigo kwa ujumla.

 

Mafunzo hayo yaliyowashirikisha watumishi kutoka mikoa ya Simiyu, Kagera, Shinyanga, Geita, Mwanza na Mara, na yalifunguiliwa na Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira wa Wizara ya Ujenzi, Mha. Kashinde Musa, aliyewaasa wafanyakazi wa mizani kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kulinda miundombiniu ya barabara na hivyo kufanya kazi kwa tija.

 

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mizani kutoka TANROADS Makao Makuu, Mha Japhet Kivuyo amesisitiza umuhimu wa watumishi wa mizani kufanya kazi kwa weledi na ubunifu ili kuelimisha na kutatua changamoto zinazowakabili wasafirishaji na hivyo kuwezesha sekta ya usafirishaji nchini kuwa na tija kwa taifa.