"SERIKALI YAJIPANGA KUFUNGA MIFUMO YA TEKNOLOJIA KWENYE MIZANI KUKABILIANA NA VITENDO VYA RUSHWA"
Mwanza
06 Mei, 2024
Serikali kupitia Wizara ya ujenzi imesema ili kukabiliana na vitendo vya rushwa imejipanga kujikita kwenye teknolojia kwa kufunga mifumo ya CCTV kamera na mifumo ya usimamizi wa taarifa kwenye maeneo yenye mizani za kupima uzito wa magari barabarani
Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira wa Wizara ya Ujenzi Mha. Kashinde Mussa amesema hayo leo tarehe 6 Mei 2024 Jijini Mwanza kwenye mafunzo kwa Wafanyakazi wapya wa mizani katika mikoa ya Kanda ya ziwa ya Mwanza, Mara, Geita, Simiyu, Kagera na Shinyanga.
Amesema mifumo hiyo itawezesha shughuli zote za mizani kufanyika kwa uwazi, ambapo Meneja wa TANROADS wa Mkoa husika ataweza kuona kile kinachofanyika kwenye kituo chake cha mzani.
Amesema kupitia mifumo hiyo TANROADS Makao Makuu, Bodi ya Mfuko wa Barabara na Wizara ya Ujenzi itakuwa na uwezo pia wa kuona kile kinachofanyika kwenye mzani na pale itakapobainika kuna uvunjivu wa sheria au viashiria vya rushwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi watu wanaohusika na vitendo vya rushwa.
Amewaasa wafanyakazi wa mizani kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kulinda miundombiniu ya barabara na kufanya kazi kwa tija.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mizani TANROADS, Makao Makuu Mha. Japhet Kivuyo amesisitiza umuhimu wa watumishi wa mizani kufanya kazi kwa weledi na ubunifu ili kutatua changamoto zinazowakabili wasafirishaji na hivyo kuwezesha sekta ya usafirishaji nchini kuwa na tija.
Aidha zoezi hilo la utoaji elimu linalofanywa na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), ni endelevu ambapo takriban wasafirishaji 2,100 katika miji na vijiji vyenye uzalishaji mkubwa wa mizigo wamepata mafunzo hayo katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2022/2023 na 2023/2024.