TANROADS YAWAKUTANISHA MADEREVA WA MAGARI MAKUBWA NA LATRA, POLISI WA USALAMA BARABARANI, JIJI LA DAR ES SALAAM
Dar es Salaam
30 Aprili, 2024
WAKALA ya Barabara Tanzania (TANROADS) imesema katika kuondokana na adha ya ukosefu wa maeneo ya maegesho Dar es Salaam inaandaa eneo la maegesho lenye uwezo wa kubeba magari 800 katika eneo la Kiluvya.
Mwakilishi wa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Clever Akilimali ametoa kauli hiyo leo tarehe 30, Aprili, 2024 alipokuwa anazungumza katika kikao kazi cha taasisi za serikali zinazohusiana na barabara pamoja na madereva kilichofanyika Dar es Salaam.
Hivi karibuni kumekuwa changamoto kubwa ya maegesho katika mkoa wa Dar es Salaam kutokana na ongezeko la malori kutoka nchi jirani zikifuata mizigo bandarini na kusababisha maeneo yaliyokuwepo kutokutosha.
"Tuna maegesho ya malori pale Kiluvya ambayo yanaweza kuchukua magari hadi 250 tulivyoona malori ni mengi tukasema tutengeneze eneo lingine la maegesho litakalobeba malori 800 ambayo itakuwa na mahitaji ya muhimu kama vyoo na bafu na ulinzi ," alisema Akilimali.
Alisema matengenezo la eneo hilo limekuwa likiendelea lakini limesitishwa kwa muda kutokana na mvua zinazonyesha lakini mvua zitakapokata ujenzi huo utaendelea ili eneo lianze kutumika mapema.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mizani wa TANROADS, Mha. Japhet Kivuyo alisema kuwa kikao kazi hicho na madereva kililenga kusikia changamoto wanazokutana nazo barabarani pamoja na maoni waliyonayo ili kuweza kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi.
Alisema madereva waliwasilisha kwao malalamiko kuhusiana na changamoto zao hivyo, katika kuzitatua wameamua kushirikiana na wadau wengine wa usafiri kama vile LATRA, Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama barabarani na Jijini la Dar es Salaam, kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo.
Aliongeza kuwa baadhi ya changamoto ambazo zimewasilishwa na madereva ni pamoja na upungufu wa maeneo ya maegesho ya magari na tozo za makosa mbalimbali.
“Ni mategemeo yetu kwamba baada ya kikao hiki washiriki watakwenda kuwa mabalozi wa kutoa elimu kwa wengine ambao hawakupata nafasi ya kuhudhuria kikao hiki na majibu waliyopata kutoka kwa wawezeshaji juu ya changamoto walizowasilisha yanafikishwa kwa wadau wengine wa usafiri barabarani,” amesema Mha. Kivuyo