News

SERIKALI YATENGA SHILINGI BILIONI 1.6 KWA AJILI YA KUWEKA TAA 308 MKOANI MARA

SERIKALI YATENGA SHILINGI BILIONI 1.6 KWA AJILI YA KUWEKA TAA 308 MKOANI MARA

Mara

13 Aprili, 2024

Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara Vedastus K. Maribe amesema katika kipindi cha Mwaka wa fedha 2023/2024; Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya kuweka taa za barabarani 308 sehemu mbalimbali za Miji na Vijiji Mkoani humo.

Amesema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kutoka Kanda ya Ziwa ambao waliokuwa na ziara ya siku tano ya kutembelea miradi ya kimakati inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita kupitia TANROADS.

Amesema “uwekeaji wa Taa katika Mkoa wa Mara ni suala endelevu, tumekuwa tukiweka taa kila mwaka kadri tunavyopata fedha lengo ni kuhakikisha kwamba Wananchi hata wakati wa usiku wanapata Mwanga na kuzuia uhalifu, watu wanapoona kuna Mwanga hata uhalifu unapungua lakini pia zitawasaidia Wananchi kufanya biashara zao, sasa hivi ukipita zile sehemu ambazo tumeweka taa Wananchi wanafanya biashara mpaka saa nne usiku’’.

Naye Msimamizi idara ya matengenezo kutoka TANROADS Mkoa wa Mara Mhandisi Fratern Shirima amesema kipande cha barabara kutoka Nyamuswa hadi Bunda tayari kumewekwa taa za barabarani na matarajio yaliyopo ni kuendelea kuweka taa hizo katika maeneo mengine.