News

SERIKALI KUJENGA DARAJA LA MITOMONI - RUVUMA

SERIKALI KUJENGA DARAJA LA MITOMONI - RUVUMA

 

Dodoma

16 Aprili, 2024

Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Wizara ya Ujenzi ipo mbioni kujenga daraja la kisasa na la kudumu kwenye mto wa Mitomoni, katika kijiji cha Mapotopoto ambalo litaunganisha Wilaya ya Songea Vijijini na Nyasa mkoani Ruvuma.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa leo tarehe 16 Aprili 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Jackiline Ngonyani, Bungeni Dodoma

“Maandalizi ya nyaraka kwa ajili ya kutangaza zabuni kwa mara ya pili kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mitomoni yapo katika hatua za mwisho na zabuni zinatarajiwa kutangazwa kabla ya mwisho wa mwezi Juni wa mwaka huu 2024”, amesema Waziri Bashungwa

Amesema zabuni za mara ya kwanza zilikamilika mwezi wa Machi 2023 lakini zilikosa ushindani kwani Mkandarasi mmoja tu ndiye aliyerudisha zabuni na bei yake ilikuwa juu hivyo sasa itatangaza tena.

Vilevile, Waziri Bashungwa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ipo pamoja na wananchi wa Wilaya ya Nyasa pamoja na Songea Vijijini, na ndio maana wanafanya juhudi ili kuweza kukamilisha manunuzi ili kumpata mkandarasi kuanza kujenga daraja la kudumu.

Aidha, Bashungwa amemhakikishia Mbunge huyo kuwa kufika mwezi wa sita hatua za manunuzi zitakuwa zimekamilika ili hatua za ujenzi wa daraja hilo ziweze kuanza.