News

RAIS SAMIA ANAENDELEA KUWEZESHA FEDHA ZA DHARURA KUKARABATI BARABARA ZILIZOHARIBIWA

RAIS SAMIA ANAENDELEA KUWEZESHA FEDHA ZA DHARURA KUKARABATI BARABARA ZILIZOHARIBIWA.


Dodoma

15 April, 2024
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipatia Wizara ya Ujenzi fedha za dharura ili kusaidia kufanya ukarabati kwenye maeneo ambayo mawasiliano ya barabara yamekatika kutokana na mvua za El-Nino zinazoendelea kunyesha hapa nchini.

Bashungwa ameeleza hayo Bungeni jijini Dodoma leo Aprili 15, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugulile aliyehoji kuhusu Mkakati wa muda mfupi wa kukarabati barabara ya Gomvu – Kimbiji – Pembamnazi ili iweze kupitika kwa gharama nafuu.

Akijibu swali hilo, Bashungwa amemuelekeza Meneja wa Wakala ya Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam kufika katika barabara hiyo na kufanya tathimini ya maeneo yote yaliyoribika ili kuhakikisha mawasiliano ya barabara yanaendelea kuwepo wakati wote.

Bashungwa amefafanua kuwa barabara ya Gomvu – Kimbiji – Pembamnazi ni sehemu ya barabara ya Mjimwema – Kimbiji - Pembamnazi yenye urefu wa kilometa 49 ambayo inajengwa kwa awamu kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha.  

“Kwa sehemu ya Cheka – Avic (km 2) tayari ujenzi umekamilika, Kwa sehemu ya Avic – Kimbiji (km 10) taratibu za manunuzi ya kumpata Mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi zinaendelea. Aidha, ujenzi kwa sehemu iliyobaki ya Kimbiji hadi Pembamnazi itajengwa kulinganana upatikanaji wa fedha”, amefafanua Bashungwa.

Kuhusu utekelezaji wa barabara ya Kibada – Mwasonga (km 41), Bashungwa amemuelekeza Mkandarasi kuanza kufanya maandalizi ya ujenzi katika eneo la mradi (Mobilization) wakati akiandaliwa taratibu za malipo ya awali pamoja na kuwajibika kuendelea kufanya matengenezo ya barabara kwasababu ashakabidhiwa barabara hiyo.