News

KATIBU MKUU UJENZI AZITAKA TAASISI ZOTE ZIANZE KUTUMIA MFUMO WA UFUATILIAJI NA TATHMINI

KATIBU MKUU UJENZI AZITAKA TAASISI ZOTE ZIANZE KUTUMIA MFUMO WA UFUATILIAJI NA TATHMINI

 

Morogoro

15 April, 2024

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Balozi,  Mhandisi Aisha Amour amewataka wakuu wa taasisi zote zilizo chini ya wizara hiyo kuanza kutumia mfumo wa kieletroniki katika ufanyaji kazi wao ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu za kisekta.

Balozi Mha. Aisha, ameyasema hayo leo tarehe 15 Aprili 2024, wakati akifungua mkutano wa  Baraza la Wafanyakazi wa wizara hiyo mkoani Morogoro.

“Niwatake kabla ya kuzindua mfumo, ndani ya wiki hii taasisi zote ziwe zimeshaanza kutumia mfumo huu na muwaelekeze watu wenu wanaosimamia mifumo waanze kuingiza taarifa zenu zote” amesema Balozi Mha. Aisha.

Vilevile, amesisitiza, Wakuu wa taasisi kuwa kwenye uzinduzi wa Mfumo kila taasisi itatakiwa kuandaa na kuhakikisha taarifa zote muhimu  zimewekwa kwenye mfumo huo. 

Aidha, Balozi Mha. Aisha ameipongeza Bodi ya Mfuko wa Barabara (Roads Fund Board), kwa kuwa Taasisi ya kwanza kuanza kutumia mfumo, ambapo hadi sasa taasisi imeshakamilisha kuingiza taarifa zake zote.

Baraza la wafanyakazi la Wizara ya ujenzi, linafanyika Mkoani Morogoro kwa siku mbili, lengo kuu ikiwa ni kujadili masuala mbalimbali na kupokea wasilisho la taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2023/24 na mpango na makisikio ya Bajeti ya Wizara ya Mwaka 2024/25.