News

TANROADS KILIMANJARO YAREJESHA MAWASILIANO BARABARA YA MOSHI - ARUSHA BAADA MAJI YA MAFURIKO YA MVUA KUJAA JUU YA DARAJA LA MTO SANYA

TANROADS KILIMANJARO YAREJESHA MAWASILIANO BARABARA YA MOSHI - ARUSHA BAADA MAJI YA MAFURIKO YA MVUA KUJAA JUU YA DARAJA LA MTO SANYA

 

Moshi

14 April, 2024

Mamia ya watumiaji wa barabara ya Moshi - Arusha wamefanikiwa kuendelea na safari baada ya kukwama kwa saa kadhaa katika eneo la kwa Msomali kufuatia Mto Sanya kujaa maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

Akizungumzia hali hiyo, Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kilimanjaro, Mha. Motta Kyando amesema chanzo cha hali hiyo ni maji kujaa pamoja na kuwepo kwa magogo juu ya daraja hilo na hivyo kusababisha magari kushindwa kupita.

Mha. Kyando amesema kwa sasa wanaendelea na taratibu za kuondoa magogo, kusafisha eneo hilo na kuimarisha tuta la barabara ili kuhakikisha barabara inapitika bila usumbufu wowote.

Amebainisha kuwa daraja lililopata changamoto hiyo ni la Sanya na sio daraja la Mto Biriri ambalo limejengwa hivi karibuni.

Tayari magari yameruhusiwa kupita upande mmoja wa daraja wakati juhudi za haraka kuimarisha na kurejesha miundombinu ya daraja hilo kwenye hali yake zikiendelea.