News

UTEKELEZAJI MRADI WA UPANUZI MLIMA KITONGA WAFIKIA ASILIMIA 25

UTEKELEZAJI MRADI WA UPANUZI MLIMA KITONGA WAFIKIA ASILIMIA 25

 

Iringa

14 April, 2024

Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imekuja suluhisho la aina mbili katika eneo la Mlima Kitonga ikiwa ni pamoja na upanuzi wa baadhi ya sehemu zenye kona kali na kuweka vioo vya usalama barabarani.

Suluhuhisho la kudumu ni kumtumia Mhandisi Mshauri ambaye atafanya usanifu wa kina ili aweze kuja na njia mbadala za kuepusha ajali na foleni mwenye mlima huo.

Akizungumza na Kipindi cha TANROADS Mkoa kwa Mkoa hivi karibuni; Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa Mha. Yudas F. Msangi amesema jumla ya kona tano (5), zenye urefu wa mita 1600 za Mlima huo zitatanuliwa, ili kupunguza ajali na foleni katika barabara kuu ya TANZAM.

Amesema kazi hiyo ni endelevu kwani inafanyika kwa kila mwaka wa fedha hadi itakapopatikana njia mbadala ambapo kutokana adha iliyopo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 6.4 kwa ajili ya uboreshaji wa Mlima huo ambao utekelezaji wake umefikia aslimia 25.

Amesema kazi hiyo inayofanywa na Mkandarasi wa Kizawa ya Mtwivila Traders and Construction Company Limited, ambayo inatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 7 inahusisha Kuchoronga mwamba, Uwekaji wa tabaka la kwanza la udongo wenye uimara Na.15 (G15) kwa unene wa Milimita 150, Tabaka la pili la udongo wenye uimara Na.45 (G45) kwa unene wa Milimita 150.

Ameeleza kuwa kazi nyingine ni kutengeneza barabara ya Zege yenye upana wa mita 4 kwenye sehemu zitakazo panuliwa, Kujenga Mifereji ya kupitishia maji ya mvua kwenye sehemu zitakazo panuliwa na kuweka Vioo (Convex Mirrors) kwenye maeneo yenye kona kali.

Wakati huo huo Mha. Msangi amesema katika kipindi cha miaka mitatu, Serikali ya awamu ya sita imetoa jumla ya Tsh. Bilioni 1.209 kwa ajili kuweka taa za barabarani 313 katika maeneo mbalimbali ya miji kwa ajili ya kuongeza usalama wa watumia barabara na kuwezesha Wananchi kufanya shughuli zao za maendeleo hata nyakati za usiku, kwa ajili ya kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na uchumi wa Taifa kwa ujumla.