News

TANROADS YAENDELEA KUREJESHA MAWASILIANO BARABARA YA IKONDA – MLANGALI BAADA YA KUFUKIWA NA MABOROMOKO YA UDONGO  

TANROADS YAENDELEA KUREJESHA MAWASILIANO BARABARA YA IKONDA – MLANGALI BAADA YA KUFUKIWA NA MABOROMOKO YA UDONGO

 

Njombe

14 April, 2024

Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoani Njombe inaendelea na kazi ya kurejesha mawasiliano ya barabara ya Ikonda – Lupila – Mlangali baada kujifunga katika eneo la Kijiji cha Masisiwe Wilayani Makete kufuatia kuporomoka kwa udongo kutoka Mlimani kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

Kufuatia hali hiyo TANROADS imepanga kujenga barabara mbadala kwa kiwango cha Changarawe kama suluhusho la kudumu ambayo itatumika kumaliza changamoto katika eneo hilo.

Katibu Tawala Mkoa wa Njombe Bi. Judica Omary ametoa tahadhari kwa wananchi wanaotumia barabara hiyo akiwaomba kutoitumia kwa muda huu wakati Serikali kupitia TANROADS wanaendelea kutafuta njia mbadala kwa kuwa mlima huo una dalili za kuendelea kushuka kwani mvua zivyoendelea kunyesha udongo nao unazidi kuwa tepetepe.

Ameeleza “Tunawashukuru TANROADS wamepambana sana na hii barabara kufungua sehemu ndogo tu kiasi kwamba watembea kwa miguu na pikipiki zinaweza kuendelea kupita’’.

Naye Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Njombe  Mha. Ruth M. Shalluah amesema kinachotokea katika barabara hiyo ya Mkoa inayounganisha Wilaya ya Makete na Ludewa ni mpasuko, kuhama na kuporomoka kwa udongo kunakosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

Amesema “kwa sasa ni eneo hatarishi TANROADS tumefika hapa na kuanza kazi ya kupasafisha tukaona mtambo unaweza kuzama ikabidi tuutoe na kutumia mbinu nyingine kwa maaana ya nguvu kazi, pia Watalaam wamezunguka eneo lote hili kuliangalia na kugundua kuwa kumeshameguka na udongo unaendelea kushuka’’

“Tumetoa taarifa kwa Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mha. Mohamed Besta na ametuhakikishia kwamba Serikali itatutengea fedha tuweze kupambana na hii hali na kuhakikisha Wananchi wanapata huduma ya kutoka eneo moja kwenda lingine" ameeleza Mha. Ruth.

Kwa upande wake, Msimamizi wa kitengo cha Matengenezo TANROADS Njombe Mha. Kipembawe Msekwa amesema barabara hiyo ya mbadala itakayokuwa kama suluhisho la kudumu, inapita katika vitongoji vya masisiwe, Iluilo, Nsoma na Ijangala ikiwa na jumla ya Km 3.43, ambapo sehemu ndogo ya barabara hiyo kwa sasa inatumika na wasafirishaji wa mbao kutoka mashambani, (sio barabara rasmi ya Tarura ama TANROADS).